MSIBA-ARUSHA
Wakati nikiwa bado naendelea kukupa safari yangu ya kanda ya Ziwa, na sasa nikiwa Mji wa Bariadi ambako kuna vijimambo kibao, ghafla asubuhi ya leo nikaamshwa na habari ya kuhuzunisha. Mashabiki, wapenzi na wachezaji wa mpira wa miguu katika Jiji la Arusha tukajikuta katika majonzi makubwa, baada ya mmoja wa walinda mlango waliokuwa katika kiwango cha juu mno kufariki dunia. Abduli, ambaye kwa wengi waliokuwa wakimfahamu vema alijulikana zaidi kama Dulla, amefariki mapema saa mbili asubuhi ya siku ya Jumatano ya tarehe 19/12/2012, wakati alipokuwa akipelekwa hospitalini kutokana na tatizo la muda lililokuwa likimsumbua la Figo. Alikuwa ni mlinda mlango wa timu ya Flamingo ya mjini Arusha. Siku chache tu kabla ya kifo chake, nami nilikuwa mmoja wa wale waliobahatika kufika nyumbani kwao, mtaa wa Jamhuri, nyumbani kwa mama Shakira na kuzungumza naye mawili matatu juu ya maendeleo ya afya yake; tukazungumza mengi na kupeana moyo kama marafiki. Lakini kwa hakika, sisi sote ni wa mwenyezi Mungu, na sote kwake tutarejea....
Sehemu ya umati wa watu waliofika mtaa wa Jamhuri, kata ya Daraja Mbili, nyumbani kwa mama Shakira kwa ajili ya msiba wa Abduli 'Dulla'. Ni mchanganyiko wa marafiki, ndugu na jamaa kutoka pande mbalimbali za Mji na nchi nzima kwa ujumla, wakiwemo wachezaji wenzake na marehemu Abduli wa timu mbalimbali za Mji wa Arusha, makocha, viongozi mbalimbali pamoja na wachezaji wengi wa zamani, akiwemo Muhidini Cheupe (mwenye fulana ya rangi nyekundu na suruali ya rangi nyeusi) aliyewahi kuwika mno miaka ya nyuma na vilabu kadhaa vya ligi kuu ya Tanzania kama Young Africans (Yanga) ya Dar es Salaam.
Hapa ni vijana mchanganyiko wa mtaa wa Jamhuri wakibadilishana mawazo pamoja na kuchangishana chochote kitu kwa ajili ya msiba wa rafiki yao.
Baada ya mwili wa marehemu kufanyiwa ibada kwenye msikiti mkubwa wa mtaa wa Jamhuri, safari ya kuelekea makaburini ikaanza, na kutufikisha katika eneo hili la makaburi linalofahamika zadi kama makaburi ya Wasomali, kilometa kadhaa kutoka mtaa wa Jamhuri; shughuli ya maziko ikaanza.
Wakati shughuli za maziko zikiendelea, wengine wakawa wamesimama pembeni na nyuso za huzuni wakitafakari hili na lile vichwani.
Baada ya mwili kuhifadhiwa kaburini, nafasi ya dua na maombi kwa ajili ya marehemu Abduli 'Dulla' pamoja na wosia kwa sisi tuliobaki hai, vikachukua nafasi...
Mwalimu Jumanne mwenye kanzu katikati ndiye aliyekuwa na jukumu hilo la dua na maombi. Pembeni ya Mwalimu Jumanne (picha ya chini) mwenye fulana ya rangi nyeupe aliyejishika usoni ni mwamuzi maarufu nchini, Sudi Abdi.
Mambo yote muhimu yalipokamilika, marafiki, ndugu, jamaa, wachezaji na hata viongozi na makocha wa timu mbalimbali za Mji wa Arusha wakaamua wapate ukumbusho pembeni ya kaburi la mpendwa wao, marehemu Abduli 'Dulla'
KISHA, watu wakaanza kutawanyika kurejea majumbani.....
Kaburi la upande wa kulia (huko waliko watu wengi) ndimo alimolazwa marehemu mlinda mlango, kijana Abduli 'Dulla'. Kaburi la mkono wa kushoto nalo ni la siku chache tu zilizopita la ofisa mtendaji ambaye nililipata jina lake moja tu kwa harakaharaka la mheshimiwa Kitumbo. Ama, kwa hakika, sisi binadamu si lolote wala si chochote ndani ya dunia hii. Rafiki yangu! Ndugu yangu! Nakuhusia uihesabu vema na kuikumbuka mno nafsi yako mwenyewe mbele ya Muumba, kabla ya siku yako kama hii isiyokuwa na saa wala jina haijakufikia kwa ghafla....! Asikudanganye mtu! Kifo hakina umri maalumu! Saa maalumu! Wala wakati fulani! Unatembea nacho tu kila siku... na kila mahali. Ama kweli, sisi sote ni wa mwenyezi Mungu, na sote kwake tutarejea....
Nahodha wako wa Mpini Wa Shoka nasema hivi, "kwa sasa, cha msingi ni kumkumbuka Abduli 'Dulla' kwa dua na maombi pekee, na wala si kwa kingine chochote kile"
....Wakati tukiendelea na shughuli za msiba huu wa Abduli, mara ghafla tu tena zikatufikia habari za kifo cha baba wa mmoja wa wachezaji wa zamani wa vilabu kadhaa vya Mji wa Arusha, Herman Methew Shirima, ambaye tulikuwa pamoja naye kwenye msiba huu wa Abduli. Baba huyo aligongwa na gari jirani na maeneo ya Usa River. Mipango ya mazishi inafanyika nyumbani kwa watoto wa marehemu, mtaa wa Jamhuri-mjini Arusha. Pole sana swahiba wangu, Herman Shirima pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wote wa marehemu Mzee Methew Shirima!
No comments:
Post a Comment