NI KWELI TUNAZIHITAJI SANA TIBA M'BADALA. LAKINI NI KWELI KILA MTU ANAZIJUA TIBA HIZO; NA ANASTAHILI KUJIUZIA TU POPOTE PALE?


Hii ni mojawapo ya meza zilizo na dawa za kiasili (za kienyeji), zikiuzwa na kunadiwa kwa kila njia. Katika siku za hivi karibuni, pameibuka makundi makubwa ya wauzaji na watembezaji wa dawa hizi za kiasili katika maeneo mbalimbali, hata ndani na nje ya nyumba za ibada na hasa misikitini. Lakini wasiwasi mkubwa wa Mpini Wa Shoka ni kwamba, ni nani hasa anayezikagua na kuzithibitisha dawa hizi kabla ya kuwafikia wanunuzi (wahitaji wenye matatizo)? Na je mtumiaji anapopatwa na madhara yoyote yale, ni kwa namna gani atasaidika? Na je ndani ya kundi hili kubwa la wauzaji wa dawa hizi, hakuna uwezekano wa kuwepo kwa wengi tu miongoni mwao walio waongo wakubwa, waliodhamiria kuisaka noti (pesa-money) kwa njia yoyote ile hata kama ni mbaya kabisa, na wakaamua kuwalisha wanadamu uchafu na vitu vingine mbalimbali visivyoeleweka kwa kisingizio (uzushi tu) kwamba ni dawa kamili zinazotibu magonjwa fulani, na kumbe ni urongo mtupu? Hivi sasa, kila mtu ni muuzaji wa dawa za kiasili, mpaka inafika mahali unashindwa kuelewa muuzaji wa kweli ni yupi, na muuzaji mwongo ni nani; kila mmoja yuko uwanjani na dawa zake zisizoeleweka usalama na ubora wake akijinadi kwa bidii kwa maelezo na maneno matamu vilivyo! Mwishowe, hata tutalishwa dawa za kulevya kwa kisingizio kwamba ni dawa za kusisimua miili, na hasa kwa wanaume ambao wengiwao wamekuwa wakilia mno juu ya ukosefu wa nguvu za kiume! Hii ni hatari tupu, jamani! Ni vema kuchukua tahadhari na kuwa makini mno, vinginevyo kuna siku utalinywa usilolijua na kumbe ni mchanganyiko wa mkojo wa mbwa na paka au vinyesi vyao, vilivyofungashwa vema ndani ya pakiti za kuvutia! Afya yako ni ya thamani mno, usiiache ikawa inachezewa chezewa ovyoovyo tu na kila uchafu. Siyo kila kinachotangazwa masikioni mwako kwamba ni dawa, na wewe unaamini tu moja kwa moja na kuanza kukibugia ukikitumbukiza kwenye mwili wako. Wajanja wamejazana uwanjani kwa ajili ya kuuza ujanja wao. Kazi ni kwako, wakwetu!

No comments: