TEMBEA UJIFUNZE, Wakwetu! ...Ama Kweli Mwenyezi Mungu Ameumba Hata Zaidi Ya Uumbaji Na Maajabu Yake!



Wageni wangu kutoka Shirika lisilo la kiserikali la MtuKwao kwa wakati huu tayari wamerejea salama salimini nyumbani mjini Mtwara. Lakini nakumbuka siku tulipokuwa njiani tukielekea Terrat-Simanjiro Manyara (wastani wa km 90 kutoka Arusha mjini) kwa ziara ya siku moja ya mafunzo kwenye kituo cha Shirika la Ilaramatak Lorkonerei, tukiwa njiani  tukiendelea na safari yetu ghafla tukayaona mashamba makubwa yaliyotawaliwa kwa sehemu kubwa na rangi ya njano. Nikawajulisha wageni wangu kwamba hilo ni zao la jamii ya Alizeti inayojulikana kama Kaltam. Lakini yenyewe ni fupi sana, na maua yake ni madogomadogo mno. Na isitoshe, ndani ya shamba hili hakuna mnyama yoyote yule anayeweza kuingia na kufanya uharibifu kwa urahisi, kwa sababu mmea huu una miba mikali. Hata wakati inapokuwa tayari imekomaa na inahitaji kuvunwa, basi hakuna uwezekano wowote ule wa kuivuna kwa mikono; ni lazima mashine ya kuvunia (harvester-combine) ndio itumike. Lakini pamoja na yote hayo, sifa kubwa ya aina hii ya alizeti (kaltam) hustawi vema kwenye eneo la nchi kame sana; haihitaji mvua kubwa; wakati wa jua kali ndipo hasa huwa inapendeza mno shambani, utadhani inamwagiliwa maji, na kumbe hapana!   

Vijana wa MtuKwao-Mtwara, kutoka kushoto Shafih Ndege, Issa Hemedi na Gregory Millanzi (aliyeinua mkono), wakiwa ndani ya shamba wakiishangaa aina hii ya Alizeti ndogo...




Hata Mohamed Massanga (mwenye fulana ya rangi ya kijani) na Salehe Kaondo (mwenye kamera), nao pia walikuwemo shambani...




Kiongozi wa msafara wao, Mkurugenzi wa MtuKwao-Mtwara, Bw. Swallah Saidi Swallah, naye pia hakutaka kuhadithiwa tu; aliingia mwenyewe katikati ya mimea hii na kuikaguakagua hapa na pale. 

Katika miaka ya 80, Mkurugenzi huyu alijipatia mafunzo yake ya ukakamavu katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa-J.K.T-Oljoro iliyopo mwendo wa kilometa chache tu jirani na shamba hili katika barabara Kuu ya Arusha-Simanjiro-Kiteto. Lakini anasema, wakati wa miaka hiyo ya 80 hapakuwepo kabisa na kilimo cha zao hili la Kaltam, ndio maana na yeye alikuwa akilishangaa.

No comments: