SOKO JIPYA! ARUSHA. UNAIJUA SEKESEKE NA PATASHIKA ILIYOTOKEA HAPA?
Mwanakwetu, zilipigwa kwanza ngumi za maana baina ya wachuuzi (wafanyabiashara ndogondogo) wenyewe kwa wenyewe wakigombea maeneo! Kwa kifupi, ilikuwa ni kama vita kamili! Ndugu zangu askari mgambo walipojichomeka ili kutaka kujaribu kulituliza patashika hilo la kufa mtu, nao wakajikuta wakiingia matatani! Kipigo cha paka mwizi kikawageukia wao; wakatimua mbio...! Kwani ni nani aliyekwambia yeye haipendi roho yake, wewe! Askari polisi nao walipofika, wakaonjeshwa kidogo joto ya jiwe kwa muda, kisha ndipo wakafanikiwa kuituliza hali ya mambo.
Wachuuzi (wafanyabiashara) hawa ni wale walioamriwa na serikali ya manispaa ya Mji wa Arusha, kwamba wasionekane kabisa wakifanya biashara zao nje ya maeneo na barabara zote zinazolizunguka soko kuu pamoja na lile la Kilombero (maarufu kama soko la matunda na samaki wabichi wa bwawa la nyumba ya Mungu). Kwa hivyo, serikali ya manispaa ikaamua kuwatengea uwanja maarufu wa N.M.C, ambao kwa kawaida umezoeleka zaidi na wakazi wa Mji wa Arusha na vitongoji vyake kama uwanja wa wazi kwa ajili ya mikutano ya hadhara na matamasha mbalimbali, na pia nyakati za jioni vijana wamekuwa wakipatumia zaidi kwa mazoezi na mechi kadhaa za mchezo wa mpira wa miguu. Sasa, ndipo ikaja hiyo siku ya Ijumaa ya tarehe 21/09/2012, wachuuzi hawa wakafika rasmi katika eneo la viwanja hivi ili kujipatia nafasi za kufanyia biashara. Hapo ndipo sekeseke, vurumai na ngumi za maana vilipozuka....!
Baada ya siku mbili tatu, sasa mambo yametulia. Maisha mapya ya kibiashara yameanza rasmi..... Si unaona mwenyewe?
Hapa hakuna kucheza mbali na eneo! Ukicheza mbali tu, unaweza ukakuta eneo limetekwa na m'babe (mtu) mwingine! Kama ni habari ya katoto ketu kachanga, tutakalea tu hapahapa uwanjani hata kwa kukafunika na mwamvuli. Njaa ikileta tabu, mwenyewe si unaliona birika kubwa la kutosha limebandikwa jikoni. Hapa habanduki mtu, mwanakwetu! Ni kuchimba mashimo na kujenga kibanda chetu cha biashara hadi kikamilike.
Pamoja na hekaheka ya kujenga vibanda, lakini Mpini Wa Shoka uliwakuta wengine wengi tu wakiwa tayari wamekwishazianza rasmi biashara zao. Huku tunajenga, na huku tunauza bidhaa. Machungwa na ndizi umeviona hivyo?
Hawa maswahiba watatu, kutoka kushoto ni Bakari Abdi `Beka` mkazi wa Mianzini, Mussa Ramadhani (katikati) mkazi wa Sakina, na Mohamed Omary `Muddy` mkazi wa Unga Limited, wao waliamua kupiga stori mbili tatu na Mpini Wa Shoka ndani ya uwanja wa soko hili jipya. Wanasema mambo sasa siyo mabaya sana. Hakuna matata tena ya mapigano wala mikwaruzano mikubwa. Waliopata maeneo wamepata, na waliokosa wamekosa, kwa sababu kwa kweli wafanyabiashara walikuwa ni wengi mno kupitiliza. Kwa hivyo, na wao wakati wakiwa katika hekaheka za kuviandaa na kuvijenga vibanda vyao vya muda katika maeneo yao waliyobahatika kuyapata, lakini kama macho yako yenyewe yanavyojionea mambo ya biashara yanaendelea kama kawa. Kapu limesheheni dagaa wa kutosha kutoka ziwa Victoria. Unataka tukupimie dagaa wa shilingi ngapi hapa? Au tukuwekee sadolini ngapi za hamu kwa ajili ya familia yako? Kazi ni kwako kufika mwenyewe kwenye soko hili jipya katika Viwanja vya N.M.C. Ni kweli tumepata sehemu mpya ya kufanyia biashara zetu, lakini hofu ya Mpini Wa Shoka ni kwamba, kwa uzoefu wa muda mrefu nilionao kwa eneo hili zima la uwanja huu (na hasa wakati ule nikisukuma gozi la ng'ombe hapa), ardhi ya hapa ni ile ya asili ya tindiga, na msimu wa mvua huwa panajaa maji mfano wa bwala la samaki aina ya kambare! Sijui kama waheshimiwa wakubwa wa serikali ya manispaa ya mji wa Arusha wanalijua vema hilo, na wamejipangaje hasa katika kuwalinda wachuuzi hawa wasije wakaadhirika, pindi vua litakapoanguka!
Hapa ni moja ya maeneo ya soko kuu la Arusha, ambako kabla ya wachuuzi (wafanyabiashara) hawa hawajaondolewa na kuamriwa kwenda kwenye uwanja wa N.M.C, kawaida palikuwa panafurika wachuuzi wadogowadogo wenye kuuza kila aina ya biashara za kushika mkononi wakitembeza, na wengine wakitandika na kupanga chini. Hapa mwenye nyanya na ngogwe...! Huku huyu na vitunguu na pilipili hoho.... na vingine na vingine...! Ilimradi hapa palikuwa hakuna hata nafasi ya kutema mate kwa uhuru kutokana na umati mkubwa wa watu uliokuwa ukijazana! Ukitema mate tu, unaweza ukajikuta umemtemea mkorofi mmoja, mara ghafla akakuanzishia balaa la aina yake la mvua ya maneno machafu yasiyokuwa na mfano, au hata ngumi zilike kabisa! Lakini sasa, kama mwenyewe unavyojionea hata magari yameegeshwa raha mustarehe. Sehemu iliyozungushiwa mabati, ni wachina wanajenga mfereji mkubwa wa maji kabla ya kuweka lami barabarani.
No comments:
Post a Comment