NDIVYO MAISHA YALIVYO.

Majengo yote haya, yapo katika Mji wa Arusha....

Hebu yatazame kwa makini, kisha jenga taswira na hisia yako yoyote ile uipendayo.





Hivi ndivyo nyoyo za wanadamu wote huwa zinatamani kuona zinajaribu kupiga hatua za kimaisha kama picha hizi jinsi zilivyopangiliwa kuanzia juu kabisa hadi chini. Yaani kutoka katika nyumba ya udongo, na kisha siku moja usogee katika hatua mpya mfano wa kuiendea picha ya pili...halafu uendelee tena mbele hatua kwa hatua hadi ikiwezekana uyafikie mafanikio mfano wa picha mbili za chini! Lakini wakati mwingine nyonyo hubaki zikitamani tu, lakini hatua hizo hazipigiki kamwe. Siku zote uko palepale, na hatua ni ngumu vilivyo kama jiwe la kusagia nafaka! Ndipo wakati mwingine unajikuta hata unajiropokea mwenyewe tu moyoni "...hivi hawa wanaosonga mbele kila siku, wao wanawezaje kusonga mbele na kuniacha mimi nimebaki katika hatua hii niliyopo miaka yote tu!" Hakika majibu ya haraka hapa huwa ni magumu mno kwa swali kama hili. Na ndipo wakati mwingine upepo wa imani mbaya huanza kuziingia nyoyo. Fikira na mawazo ya kila aina yatapeperuka ovyo huku na kule kwa kishindo ndani ya ubongo. Mpini Wa Shoka wenyewe unasema hivi, "siku zote katika maisha, usipoteze muda wako kusema eti sisi hatuna pesa. Sema, mimi fulani ndiye sina pesa". Kama watu wote mjini wasingekuwa na pesa, basi makazi na majengo yote mji mzima yangekuwa mfano wa picha ya kwanza kabisa juu. Usijipotezee bure muda na umri wako kwa porojo nyingi zisizokuwa na faida juu ya mali na uwezo wa wengine. Fikiria kwa makini ni jinsi gani na wewe utajaribu kupiga hatua moja hadi nyingine katika kusonga mbele juu ya harakati zako, japo kidogo tu.      

No comments: