MAMBO YA MICHEZO HAYA.

Siku ya Jumamosi (29/09/2012), ndani ya uwanja wa michezo wa Sheikh Amri Abeid kuanzia saa 10 za jioni kutakuwa na mechi ya mpira wa miguu ya ligi kuu ya Tanzania kati ya wenyeji timu ya JKT-Oljoro dhidi ya Mgambo Shooting.  Jioni moja (siku moja) kabla ya mechi hii, Mpini Wa Shoka ulizama ndani ya uwanja huu ukakuta mazoezi ya michezo kadhaa ikifanyika, hasa netiboli (mpira wa pete), Volleyball na Kick boxing (ngumi teke). Lakini tamu ilikuwa ni hii hapa. Huyu jamaa alikuwa amejimix vilivyo na akina dada akicheza nao netiboli (mpira wa pete) akiwaonesha viwango vya kufa mtu.... Jionee mwenyewe!


                        Wenyewe walimwita 'ticha'.



   Alikuwa akiwakamua vilivyo wakina dada kwa viwango.



Hapa anaomba pasi kutoka kwa mwenzake mwenye fulana ya rangi ya pinki, huku akiwa amezungukwa na walinzi watatu wanaomkaba. Ilikuwa ni hekaheka tupu. 



Amefanikiwa kuwatoroka walinzi waliokuwa wakimlinda; hapa anafanya kweli. Unaviona vitu vyake? Shabaha za hatari!                                         




    Hapa anarudi taratibu kati, baada ya kutupia pointi (pete). Hata mimi nakumbuka wakati nikicheza soka katika ligi mbalimbali za mkoa wa Arusha, niliwahi kucheza na dada mmoja aitwaye Pili katika klabu maarufu cha Jamhuri F.C, ambaye wakati huo alikuwa ni hatari kwelikweli mazoezini kwa chenga za maudhi, kiasi ambacho hata baadhi ya mabeki wa timu walikuwa wakimhofia. Wakati huo nilikuwa nahodha wa timu hiyo nikiwa na wakali wengi tu kama mlinda mlango Aldina Hashim aliyepata kuzichezea timu za ligi kuu za A.F.C ya Arusha na Mtibwa Sugar ya Manungu-Morogoro, pamoja na marehemu Nadhir Mussa Mchomba, aliyefia uwanjani akiichezea A.F.C. Sijui hata siku hizi yule Pili machachari yuko wapi tena! Majukumu.  



HAPA NAPO.....

Watu wazima walikuwa wakichuana katika mazoezi ya Volleyball.



 Kama katika maisha yako ya utoto na ujana haukuwa na tabia ya kushiriki michezo, basi siku utakayojichomeka na wewe kutaka kuonesha uwezo wako, tambua ni lazima tu siku hiyo utageuka kituko. Mpira kama huu kwako utakuwa ni sawa na sungura anayefukuzana na mbwa! Hautulii wala haukamatiki kirahisi! Si unajionea mwenyewe mambo hapo juu!


HAPA IKAWA....

          Ni kazi ya kujifua vilivyo. Ni miondoko ya ngumi teke (Kickboxing)



 Kila jambo linataka maandalizi ya ukweli kama hivi, kabla ya kuelekea kwenye mashindano yoyote yale. Siyo kujikurupukia tu. Utaoteshwa manundu ya kutosha usoni, mwanakwetu. Ohooo! Shauri yako!

                                                                         

KWENYE VIBANDA UMIZA NAKO....

   Jumamosi hii (29/09/2012) huku na huko katika mji wote wa Arusha, mabango yanaonesha uwepo wa hekaheka za mechi kadhaa za mchezo wa mpira wa miguu, na hasa huko nchini Uingereza kunako mashabiki wengi. Lakini kali na kubwa kabisa ambayo macho na masikio yataelekezwa kwa nguvu zote ni ile kati ya Arsenal na Chelsea. 

  Shabikia sana, lakini usipitilize sana hata ukajisahau kwamba yupo aliyekuumba, na unahitajika kumkumbuka na kumshukuru japo kidogo. Dunia tambara bovu, mwanakwetu; tunavunwa na mwenyewe kila sekunde kama mchicha! Au wewe hauna hiyo habari!  

No comments: