MUSOMA MJINI.

Safari yangu ikanipeleka hadi Mji wa Musoma, kwa wajomba zangu. (Siku nitakyokwenda kwa Shangazi zangu; Morogoro, natumaini nako pia nitakupa vitu kibao)


Hapa ni eneo linalojulikana kama Rwamlimi, ambako ndiko bi mkubwa wangu (mama yangu mzazi) anakoishi. Ukanda wa maji ya Ziwa Victoria unaonekana vema.




Bi mkubwa wangu, Zuhura Hussein Jigge, aliyejitanda ushungi akanipokea kwa raha na bashasha zote na ndugu yake, dada Agnes. Kwa bi mkubwa wangu huyu hata kama mfukoni nimecharara vilivyo, huwa napokelewa vema tu kwa furaha zote. Kawaida yangu kwake huwa sichezi mbali na samaki sato wa kuchemsha ama wa kukaanga, au hata sangara, ningu, mumi, gogogo na.... Hey! mbona umeduwaa kwa hayo majina? Usiogope; ni majina tu ya samaki ndani ya Ziwa Victoria. Wote hao ni watamu vilivyo kwa ugali mkubwa wa muhogo na mahindi au hata asubuhi kwa viazi vitamu vya kuchemsha (heavy breakfast), wenyewe wa Musoma wanaviita Numbu. Ni utamu mtupu kwa kwenda mbele, katumbo ndiiiiiiii!

 

 

Huyu siyo Kenge wakwetu. Mojawapo ya vitu ambavyo huwa vinanivutia sana katika Mji huu wa Musoma ni aina hii ya Mijusi. Wanavutia sana; maisha yao wakati wote ni kwenye mawe na vichwa vyao mara zote huwa havitulii; vinachezacheza huku na kule; chini juu chini juu. Mwenye rangi za aina hii huwa ni dume. Majike huwa na rangi moja tu kama ya mbao.



Hapa ni nyumbani kwa mmoja wa maanko zangu, Omari Mustafa Jigge, aliyekaa kulia akiwa na baadhi ya watoto zake, Malima aliyejifunga kitambaa shingoni, na Mwajuma "Mwaju" katikati. 

 

 

ZIZI LA BATA!

Nyumbani kwa Anko Omari Mustafa Jigge. Wakati wote huenda umezoea kusikia kwamba kuna zizi la mbuzi... zizi la ng'ombe... zizi la Punda au hata zizi la Farasi. Lakini hapa mjini Musoma Mpini Wa Shoka umeshuhudia kuliona zizi la Bata. Wamo ndani ya Zizi lao! Hapa huzuiliwa kwa nyakati za mchana ili wasilete usumbufu. Kwa hivyo mambo ya chakula na maji huwa ni hapa hapa. Na kwa kuhara hawa jamaa si wanafahamika vema. Kwa hivyo wakizuiliwa kwa namna hii, inaweza ikasaidia mambo ya usafi. Ndio maana waswahili wanakajimsemo kao kwamba 'kunya anye kuku, akinya bata eti yeye kaharisha.....!' Unaionaje hii staili ya Zizi la bata! Inakufaa na wewe?

 



Anaitwa Anko Jailani Omary kushoto akiwa kazini na kijana wake, mjini Musoma. Mambo ya miundo mbinu ya maji taka. Ukikosea tu, nyumba yote inanuka.




Katika pitapita zangu katika eneo hili la Rwamlimi, mara ghafla siku moja nyakati za jioni nikalifuma kundi hili la vijana likiserebuka vilivyo....

Kumbe hii ni timu ya mpira wa miguu iliyokuwa ikijiandaa kufanya mazoezi katika eneo hili. Lakini ghafla tu ikapita habari kwamba mpira wanaoutumia kuna dharura iliyotokea, kwa hivyo jioni hiyo usingepatikana kwa ajili ya mazoezi yao. Ndipo badala ya kufanya mazoezi ya mpira wa miguu, mmojawao akawasha muziki mzito kwenye simu yake (sielewi hata ilikuwa ni simu ya kichina au ni ya kihindi; miye sijui maana muziki wake ulikuwa ni kama disco kamili), kazi ya kuserebuka ikaanza. Kila mmojawao akionesha ufundi na ujuzi wake! Hapa yupo Kulwa, Massawe, Adam na Obadia. Kazi ni moja tu vijana wa kwa-Rwamlimi. 

No comments: