SAFARINI-KANDA YA ZIWA
Habari za siku kadhaa wa kadhaa za kupotezana, wakwetu. Mpini Wa Shoka ulikuaga; japo sikukueleza wazi ni wapi ninakoelekea. Nilitegemea huenda ningerejea mapema sana katika Mji wa Arusha, lakini wapi! Ama kweli safari ni hatua; mara zote unaelewa vema pale unakotoka, lakini kule unakokwenda kwa hakika haujui ni kipi kitakachokukuta. Huko nilikokwenda nimekukusanyia mambo kibao chungu wa tele. Jitahidi tu kila siku kuufuatilia Mpini Wa Shoka utaipata vema 'hadithi' ya safari yangu kwa jicho lako.
Na hivi ndivyo nilivyoianza .....
Ndani ya basi nililosafiria, Mpini Wa Shoka ulikuwa macho. Hapa ni kwa mwonekana wa mbali tukiwa kwenye vilima vya kuelekea Kilimatembo-Karatu, linaonekana Ziwa Manyara; jirani na Mji wa Mto Wa Mbu.
HAPA ni kwenye geti kuu la kuingilia mbugani (Ngorongoro)
Mambo ni mchanganyiko tu wa kila namna. Wazungu kwa waafrika... wahindi kwa waarabu....hata wachina na wajapani; sote tuko safari moja.
Safarini ndani ya mbuga. Hapa ni katika mwinuko mkali wenye miteremko ya hatari inayotisha mno iliyo jirani kabisa na kreta (Ngorongoro Crater). Hizi ni nyakati za asubuhi, ukungu mzito umetanda njia nzima. Dereva asipokuwa mjuzi tena aliye makini, basi ni hatari kubwa. Panafahamika zaidi kama vilima vya Malanja (Malanja Hill). Kama una roho nyepesi, funga macho wakwetu; mwache dereva apige gia!
Kwenye tambarare ya mbuga ya Ngorongoro, kuna vivutio vya wenyeji vinavyofahamika kama boma. Watalii hupata fursa ya kununua vitu vya asili hapa, kuchezewa ngoma na kujifunza mambo mengi tu kuhusiana na mila, tamaduni na desturi za wananchi wa jamii ya kimaasai wanaoishi sambamba na wanyamapori kama simba na chui ndani ya hifadhi bila ya hofu wala shaka yoyote ile!
HAPA ni kwenye tambarare ndefu ya mbuga ya Serengeti. Wakati basi likiwa kwenye mwendo mkali, hakuna nafasi ya kujiandaa kuchukua picha! Ni uwezo wako tu. Vinginevyo hauambulii kitu. Mpini Wa Shoka ulijitahidi kujituma kwa kila hali.....
Swala wakiwa malishoni
Nyumbu wakilimbia basi tulilosafiria. Hawa jamaa yaani mbugani ni wengi ile mbaya! Utadhani mbuga yote ni yao peke yao! Unaonaje kama hawa wote wangekuwa ni ng'ombe wako unaowamiliki kwenye zizi lako. Mambo yangekuwa safi!
Acha kabisa weye! Ama kwa hakika Mungu ameumba kwa viwango visivyokadirika wala kupimika. Hebu tazama jinsi hawa jamaa wanavyopendeza...wanavyovutia machoni. Ni kundi la Pundamilia (Zebra).
TUKAFIKA kituo (geti) cha Naabi. Tukapumzika kidogo kwa ukaguzi na kujisaidia a.k.a 'kuchimba dawa'. Uchimbaji wa dawa ndani ya hifadhi za wanyama siyo mahali popote tu kama wewe ulivyozoea hapo mtaani kwenu. Kuna maeneo maalumu. Faini yake utakoma mwenyewe. Hairuhusiwi hata kutupa taka. Shauri yako.
Hiki ndicho chombo chetu tulichokuwa tukisafiria. Hapa Naabi gate tulipata pancha kidogo; ikashughulikiwa.
NAABI GATE
Hata watalii nao tuliwakuta wamejipumzisha hapa Naabi gate, wengine wakipata maakuli kabla ya kuendelea na safari zao za utalii. Wengine hapa walikuwa ni vi-babu na vi-bibi vizee kabisa, lakini wamekuja Tanzania kuinjoi laif wakwetu. Na wewe utainjoi lini? Au na wewe hadi uzeeke kabisa!
TUKAENDELEA na safari kwa kasi....
Tukafika Seronera. Hapa wakwetu, tulikaa karibu saa nzima mataili mawili yaliyopata tena pancha yakishughulikiwa. Wengine hata wakajivutia viti na kujipumzisha kabisa.
BAADA ya matengenezo, tukasonga mbele.
Mwendo mfupi tu baada ya kuiacha Seronera wakati tukiitafuta Fort Ikoma (geti la mwisho la hifadhi ya Serengeti), ghafla kwenye bonde moja Mpini Wa Shoka ukalifuma hili jibaba (Kiboko) limetoka ndani ya maji linakula majani. Raha tupu.
Hapa ni mji wa Robanda baada ya kutoka ndani ya hifadhi. Biznes zinaendelea kama kawa.
KISHA....
Kwenye saa kumi na moja na madakika kadhaa hivi jioni tukatua Makao Makuu ya wilaya ya Serengeti; Mji wa Mugumu; Hapa Pamekucha ile mbaya wa kwetu.
No comments:
Post a Comment