JUMAPILI 26/05/2013. Viwanja vya Msikiti Mkuu-Arusha
Mwongozaji wa kongamano hili, Imam Hambal wa
Msikiti Mkuu Arusha, akisisitiza jambo na hasa juu ya kuwataka waislamu kuwa
imara na kujitambua, kwani sasa kila ubaya wowote ule unapotendeka tu ndani ya
nchi ya Tanzania, basi uzushi na vidole vyote vya lawama na shutuma vinaelekezwa
kwao, hata kama aliyetenda ubaya huo siyo
mwislamu.
Palipo na wakubwa hapaharibiki jambo. Mmoja wa wazee wa Kiislamu, Mzee Issa Kieti, waliopewa nafasi ya kuwasalimia waliohudhuria katika kongamano hili
Mwenyekiti wa Shura ya maimam wa Arusha (Ahal Sunna Wal Jamaah) Sheikh Mohammed
Ramadhani wa msikiti wa Sakina-Maziwa, akielezea umuhimu wa amani kwa
watanzania wote, na jinsi uislamu kwa mujibu wa Qur’an tukufu na hadithi za
mtume Muhamad unavyokataza matendo ya uuaji, uonevu, unyanyasaji na uharibifu
wa mali kwa kisingizio cha namna yoyote ile. Na jinsi hata Mtume Muhammad
(s.a.w) mwenyewe namna alivyoishi kwa maelewano na mashirikiano na watu wengine
wasiokuwa waislamu katika enzi za zama zake.
Amir Swalahudin, kiongozi wa tabligh, naye pia alipata fursa ya kufafanua
masuala kadhaa, na hasa juu ya uchochezi unaopitishwa kwa nguvu kisiasa ndani
ya nyumba za kidini, ili kuuchafua na kuupaka matope uislamu, likiwemo tukio la
mlipuko wa bomu kwenye Kanisa Katoliki Parokia ya Olasiti mjini Arusha, ambapo
katika wiki nzima baada ya kutokea kwa tukio hilo waislamu walishambuliwa kwa
maneno ya shutuma na kulaaniwa vikali waziwazi mitaani, ndani ya vyombo vya usafiri na hata kwenye maofisi ya binafsi
na yale ya Serikali kwamba wao hasa ndio wanaohusika na tukio hilo, na hawafai
kabisa kuwemo ndani ya jamii ya watu wa taifa la Tanzania…
Waandishi wa habari na wapiga picha nao pia
walikuwepo kwa wingi. Huyu ni mmojawao, Bw. Twaha Hussein Saidi, akiwa katika harakati za kunasa picha kadhaa za
matukio.
Hata viongozi wa misikiti kadhaa ya Mji wa
Arusha nao pia walihudhuria kwa wingi. Hawa ni baadhi yao. Ni viongozi vijana kabisa wa
msikiti wa Taqwa, uliopo katika kata ya Daraja Mbili. Kutoka kushoto ni Kawawa Mohamedy Jailosy Kawawa (Katibu
wa msikiti) na Ustaadh Mohamed Ismaili Kilongo (aliyevaa kanzu), Imam msaidizi.
Katika kongamano hili, pia walialikwa viongozi kadhaa wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bwana Magesa Molongo, pamoja na Kamanda Mkuu wa Polisi wa mkoa wa Arusha. Lakini hata hivyo kwa bahati mbaya sana, viongozi wote hawa waliomba udhuru kwani walikuwa wameitwa katika kikao cha dharura na Waziri Mkuu Mh. Mizengo Kayanza Peter Pinda.
Lakini hilo halikuzuia tamko la waislamu wa Mkoa wa Arusha kusomwa hadharani (likiwa limepewa baraka zote za kusomwa na Mkuu mwenyewe wa Mkoa wa Arusha, Magesa Molongo, japo yuko safarini)…
Sheikh Mustafa Kihago ndiye aliyekuwa na jukumu hilo la kulisoma tamko hilo, ambalo limelaani waziwazi
tukio la mlipuko wa Kanisa Katoliki-Olasiti, Arusha, lakini likiwaonya
wanasiasa na viongozi wa kidini, hasa wa kikristo kuacha kuwanyooshea vidole
waislamu, kwani kwa kufanya hivyo wajue wazi wanachochea chuki, wakati ushahidi wa jambo hilo kwamba waislamu ndio
waliohusika hawana. Tamko hilo
lilikwenda mbali zaidi, kwa kutolea mfano wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda jinsi chanzo
chake kilivyoanza taratibu kwa chochoko za kutuhumiana hapa na pale,
zikichochewa na wanasiasa pamoja na vyombo vya habari, na mwisho wake wanyarwanda
wakafikia hatua ya juu kabisa barani Afrika, ya kuuana na kuchinjana ovyo kama kuku.
Waliohudhuria wakisikiliza kwa makini wakati tamko likisomwa na Sheikh Mustafa Kihago...
No comments:
Post a Comment