AMA KWELI, MNYONGE MNYONGENI; HATA KAMA HAKI IKO UPANDE WAKE, ATANYONGEWA CHINI TU..!


Mpini Wa Shoka ulikuwa umeegemea mojawapo ya nguzo za umeme ukiwa hauna hili wala lile katika eneo la Unga Limited (ndani ya Jiji la Arusha) ukimsubiri rafiki yake mmoja aliyekuwa akiendesha pikipiki ili waelekee pande za katikati ya Mji kwa ajili ya shughuli yetu fulani hivi, ndipo ghafla tu pakatokea mkasa huu... 


Kijana aliyevaa fulana ya rangi nyeupe alikuwa akipita pembezoni mwa barabara akiendesha mkokoteni wake uliokuwa na miwa aliyokuwa akiiuza kwa bei ya rejareja katika maeneo haya ya Unga Limited. Ndipo wakati akipishana na lori la rangi ya kijani la kubebea maji machafu linaloonekana kwa pembeni, likaupamia mkokoteni wake ukabomoka kama unavyouona. Aliyeshika kiuno ni mmoja wa wahusika wa gari aliyeteremka haraka baada tu ya ajali kutokea.  




Baada ya majibizano mawilimatatu, wakaamua waubebe mkokoteni wauondoshe barabarani ili usisababishe msongamano (jam) wa magari. Mhusika mwingine wa kwenye gari (aliyeweka mikono mgongoni), naye pia akateremka kutoka kwenye gari. Ndani ya gari akabaki dereva peke yake...  




Katika hali iliyouacha Mpini Wa Shoka na maswali chungu nzima kichwani, ni pale tu walipofanikiwa kuuondosha mkokoteni kutoka barabarani na kuuweka kando (pembeni), jamaa wahusika wa gari walimgeuzia kibao (walimbadilikia) kijana wa mkokoteni kwa kumwambia kwamba yeye ndiye aliyekuwa na makosa katika tukio la ajali hii; kisha wakadandia ndani ya gari lao, haooooooooo wakatimua zao vumbi na gari lao, wakatokomea; wakamwacha kijana huyu akiwa amezubaa na kuchanganyikiwa ghafla asijue la kufanya! Sasa hapa, kwa siku hii unafikiri alitakiwa afanye kitu gani hasa! Aupeleke mkokoteni kwa fundi ukatengenezwe, Au aendelee tu kuuza miwa yake hata kwa kuibeba mabegani hadi pale itakapomalizika, ndipo afanye utaratibu wa kuushughulikia mkokoteni kwa fundi? Ama kweli mnyonge ni mnyonge tu, hata kama haki iko upande wake atanyongewa chini tu....

Mpini Wa Shoka nao ulidandia pikipiki ya rafiki yake na kutimkia town, na kumwacha kijana pembeni ya vifusi vya mchanga akipanga mbinu za kutoka hapa!

No comments: