MAISHA NI POPOTE; KAMBI NI KOKOTE, Mwaketu! BORA TONGE LA WATOTO NA ADA ZAO ZA SHULE ZIPATIKANE..! VINGINEVYO, AMANI NDANI YA NYUMBA IKO SHAKANI....


Ni mmoja wa madereva teksi maarufu na wa siku nyingi mno ndani ya Jiji la Arusha na vitongoji vyake. Mpini Wa Shoka umeanza kumfahamu miaka mingi tu iliyopita, wakati fulani tukipiga kazi na kikosi-kazi cha nguvu cha wana-Redio 5 Stereo, kwenye jengo la CCM-Mkoa wa Arusha; jirani kabisa na uwanja wa michezo wa Sheikh Amri Abeid na pia jengo la makumbusho ya Azimio la Arusha. Aisee! Ni siku nyingi sana, hata kabla Mji wa Arusha haujafikiriwa kamwe kwamba iko siku utaitwa Jiji...! Huyu jamaa wakati huo na teksi yake alikuwa akiegesha (kituo) pembeni mwa jengo la CCM-Mkoa wa Arusha. Kwa miaka ya hivi karibuni, Mpini Wa Shoka umekuwa ukimkuta mara kwa mara katika eneo hili jipya, ambalo kwa wakazi na wenyeji wa Mji wa Arusha wanapafahamu vema kwa jina la 'Stendi ya Dar Express'. Ni Jirani na hospitali ya kisasa ya Selian...  


Jina lake halisi anaitwa Deogratius Mwambilwang'wazi 'Deo', ambaye kwa madereva wenzake wa teksi na watu wengine wanaomfahamu vema katika Kituo hiki cha mabasi (stendi ya Dar-Express), anafahamika zaidi kwa jina maarufu la 'mzungu'. Wewe mwenyewe si unamwona vema jinsi alivyo mweupe, hata zaidi ya hilo basi lililopo kushoto pake! Duniani kuna vimbwanga bwana; haya ndio mambo ya Arusha City!   




Hapa ndipo eneo lenyewe la kituo hiki cha mabasi (stendi ya Dar Express). Ni jengo la Shirika la Nyuma la Taifa (National Housing). Hapa yanapatikana mabasi ya kwenda Tabora, Musoma, Mbeya, Morogoro, Dar es Salaam na maeneo mengine kadhaa ya Tanzania. Usafiri wa boti wa kwenda visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba, ndio pekee haupo hapa!




Bwana braza-kaka Deo 'Mzungu' akiongea kwa ufupi tu na Mpini Wa Shoka, anasema, "Kwa kweli, tunamshukuru Mungu. Hapa (katika kituo hiki) kazi siyo mbaya sana; Mungu anasaidia...". Nyuma yake, basi maarufu la CoastLine linalokwenda Tabora likipakiza mizigo ya abiria wake wakati wa jioni kwa ajili ya safari ya siku inayofuata (mapema saa 12 za asubuhi linaanza kutimua mwendo). Ukiupenda sana usingizi kitandani, basi ujue utabaki na tiketi yako mkononi ukiwa umeachwa kwenye mataa. Abiria wengine kwa kuepuka kuachwa, huwa wanaamua kulala ndani ya basi hadi hiyo asubuhi ya safari. 

No comments: