Wakwetu! WACHINA BADO WAPO NDANI YA JIJI LA ARUSHA. BADO WANAENDELEA KUFANYA KWELI KATIKA KUZIBORESHA BARABARA NA MITAA....


Kama kuna barabara zilizokuwa zimeoza na kuchakaa vilivyo, na kuwa ni kero na udhia usio na mfano kwa ubovu wake wa miaka mingi ndani ya Mji wa Arusha, basi miongoni mwao ni hii barabara Kuu ya eneo la Majengo. Barabara hii kwa sasa imekwishafanyiwa kazi maridadi na wenzetu kutoka Jamhuri ya watu wa China, ambapo tayari wamekwisha ilambisha lami maridadi. Barabara hii inaanzia Majengo kwenye makutano ya barabara ya Sokoine (Barabara ya Arusha-Dodoma) na kwenda hadi eneo la Azimio (Sakina) kwenye Barabara Kuu ya Arusha-Namanga-Nairobi. Kwa hivyo, japo wachina bado wanaendelea na kazi za ujenzi, hasa kwa mitaro na makaravati pembezoni mwa barabara hii, lakini kwa sasa ni mterezo tu (mkeka laini) kwa madereva wa vyombo vya moto kutokea Azimio (Sakina) hadi Majengo....       


Huko macho yako yaliponyookea, ni upande wa kuelekea Azimio (Sakina). Tazama kwa makini mbele kabisa utauona mwonekano wa Mlima Meru kwa mbaaaaaaali.





Na huku yanakoelekea magari na pikipiki, ni kwenye makutano ya barabara hii ya Majengo na barabara ya Sokoine (Barabara ya Arusha-Dodoma)

 

 

 

Hapa ni kwa upande wa kutokea Azimio; unateremka kuelekea pande za Majengo...

Hii ni moja ya kona kali baada tu ya kukipita Chuo cha masuala ya Kompyuta cha JR Institute-Azimio.  Gari hilo dogo la rangi nyeupe linatokea pande za Majengo. 




Hapa tunaelekea eneo la kanisani penye mteremko mkali. Upande wa kushoto anakoonekana mwanafunzi, kuna shule ya Msingi na Sekondari. Zamani (kabla ya wachina hawajaishughulikia barabara hii), hapa palikuwa na kona moja kali sana ambayo mara kadhaa iliyasababisha magari kukosana chupuchupu kugongana ama kugongana kabisa. Kona yenyewe ya barabara ya zamani ni hapo unapoliona hilo gari limetokeza, ambapo wakati wa enzi hizo lingelazimika kukata kona kali upande wa kulia kwa kuifuata barabara inayoambaa ambaa pembezoni mwa nguzo ya umeme inayoonekana vema (kulia kabisa). Nakumbuka hapa palikuwa ni mojawapo ya mahali pa hatari mno. Hongera sana wachina kwa kuiona hatari hiyo na kuiondosha...    




Hapa ndipo eneo la kanisani (mteremkoni kuelekea Majengo). Pana kajieneo kafupi tu hapa ambako ndiko bado hakajawekwa lami mbele kidogo mwa Kanisa linaloonekana kushoto 

 

 

 

Barabara Kuu ya eneo la Majengo imechapwa lami maridadi kwelikweli kama unavyojionea mwenyewe kwenye picha za hapo juu, lakini barabara zote za mitaa na vitongoji vya eneo hili bado zipo katika hali ngumu mno, na hasa pale mvua inapoanguka ndipo utakapoelewa vema kile ambacho Mpini Wa Shoka unamaanisha... Sebene (kasheshe) lake hapa, hasa kwa wenye vyombo vya moto, huwa siyo la kitoto! Ni hatari ya denja (danger), Mwakwetu! 

Hii ni mojawapo ya barabara hizo za mitaa na vitongoji vya Majengo. Watu wanaendelea na Mishemishe (pilikapilika) zao za kawaida. Huko wanakoelekea hao wanamume wawili wenye mashati ya rangi nyeusi, ndipo ilipo barabara Kuu iliyochapwa lami... Ni mwendo wa hatua kadhaa tu.

No comments: