MJI WA LAMADI

Nikiwa mjini Musoma, ghafla nikafikiwa na taarifa za kushitusha kwamba mmoja wa mama zangu amefariki dunia katika Mji wa Bariadi; Mkoa mpya wa Simiyu. Ikanibidi mimi na bi mkubwa wangu (mama) tufunge safari ya kwenda kwenye msiba. Katika safari hii tukapitia miji mingi tu ya njiani ukiwemo Mji wa Bunda tukitumia barabara kuu ya Musoma-Mwanza. Na tulipofika katika Mji wa Lamadi, ndipo tukaiacha barabara hii kubwa ya Musoma-Mwanza na kuchukua usafiri mwingine wa kuelekea Bariadi. Wakati nikiwa katika Mji huu wa Lamadi, sikuacha kuokota mbili tatu. Na kilichouvutia zaidi Mpini Wa Shoka katika Mji huu mdogo wa Lamadi, ni pilikapilika na harakati nyingi za huku na kule za wakazi wake. Kwa ufupi, ni kajimji kalikokucha kwelikweli kwa hekaheka....... 


      Stendi iko barabarani kabisa; ni biashara na usafiri wa kila aina.



                                                   KITOWEO SOKONI.

Samaki fresh kutoka Ziwa Victoria. Soko la samaki-Lamadi. Wafanyabiashara kazini. Mezani kama unavyojionea mwenyewe kuna Sato, mumi a.k.a kambare, na kadhalika. 



                             Hapa ni Sato na kamongo(aliyepasuliwa).

 


 Wakwetu, hizi siyo ngozi za ng'ombe, mbuzi, kondoo au za nyumbu zimetundikwa! Hapana. Hizi ni samaki. Samaki yoyote yule mkubwa anaweza akachanwa kwa mtindo huu kisha akakaushwa kama unavyojionea. Wenyewe wakazi wa kanda ya ziwa wanaviita vibambara. Wakwetu ni vitamu hivyo kwa ugali, yaani wee acha tu! Nikununulie kimoja? 

 

 

 Baada ya kutoka Mji wa Lamadi, safari ya kuelekea Bariadi ikaanza....

 Huenda bango hili baada ya muda maelekezo yake yatabadilishwa. Kwa sababu tayari eneo hili kwa mujibu wa wenyeji, kwa sasa liko ndani ya mkoa mpya wa Simiyu ambao makao yake makuu ni Mji wa Bariadi, badala ya wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza. Hapa watu wanapiga jembe siyo kidogo. Mahindi yamekubali kwelikweli. Tazama picha ya chini. Ni mashamba yaliyopo pembezoni mwa barabara kuu ya Lamadi-Bariadi, barabara ambayo inaendelea kutengenezwa kwa kiwango cha lami.


No comments: