MAMBO YA DRAFT!

Kuna asili zingine za utani zinawahitaji watani wenyewe kwa wenyewe wafanyiane huo utani. Na tena watani hao wanahitajika kuwa na uvumilivu pamoja na ustahamilivu wa hali ya juu mno ndani ya nyoyo zao. Vinginevyo, mtu anaweza akachomoka ghafla na panga au silaha nyingine yoyote ile ya hatari mkononi na kumdhuru mtu au watu fulani wanaomfanyia utani kama huu unaoonekana kwenye picha hapa chini! Katika pitapita za Mpini wa Shoka katika mitaa na vitongoji vya Mji wa Arusha, mara ukafika mtaa wa Jamhuri (Jaluo) uliopo katika kata ya Daraja Mbili na kukutana na utani huu wa wacheza bao (draft)...  hivi kama ingelikuwa ni wewe ingelikuwa vipi hapa? Lakini mmoja wa wahusika wenyewe aliyefanyiwa utani huu ndiye aliyenipa ruksa ya kuiweka habari hii kwenye ukurasa huu ili na wewe ujionjee utamu.... 

 

....kwenye mchezo wa bao (draft), kupigwa (kufungwa) supa huwa ni sawasawa na kupigwa magoli 12 kwa mechi 1 tu! Kwa hivyo, huwa ni kitendo cha kufedhehesha sana. Hata mimi japo siuwezi vizuri mchezo huu wa bao (draft), lakini kuna mwaka fulani niliwahi kumfumania bingwa mmoja aliyenijia kichwakichwa na kumchapa Supa; kisha nikagoma kucheza naye tena ili nisije nikaumbuka wakwetu!




Vijana Mustafa (kushoto) na Stivin wakiwa katika mpambano mkali wa bao (draft) mtaa wa Jamhuri. Mmoja wa waliyopigwa Supa na kubandikwa kwenye tangazo (picha za juu) ndiye huyo aliyesimama na shati lake jeupe. Sasa sielewi hapa anamwelekeza yupi kati ya hawa wawili, baada ya yeye kulambishwa supa!

 

 

"Braza kaka, Obedi, cheza basi na jezi yako nyeupe! Sukuma kete, muda unakwenda. Kama vipi, kubali kwamba hapa tayari nimeshakuumiza (nimekupiga bao). Vinginevyo, na wewe angalia nisije nikakulambisha Supa ukabandikwa kwenye ubao wa matangazo kama hao wenzio ambao tayari wamekwishabandikwa."

No comments: