USINGIZI UKIKUBANA VILIVYO, BASI UNAWEZA UKAJIKUTA UKILALA FOFOFO TU HATA JUU YA MASHINE YA KUSAGA INAYOUNGURUMA KWA SAUTI KUBWA!
Hiki ni kichaka kikubwa cha maua pembezoni mwa barabara Kuu ya Arusha-Moshi, eneo la King'ori. Mpini Wa Shoka mapema asubuhi ulimfuma mtu huyu akiwa ameuchapa usingizi vilivyo ndani ya kichaka hiki bila ya hofu wala wasiwasi wowote ule! Mwanzo jicho langu lilipomwona, nilihisi labda ulikuwa ni mwili wa maiti uliotupiwa ndani ya kichaka hiki! Lakini alipojigeuza kidogo, ndipo nikatambua kwamba alikuwa hai kabisa akiwa ameuchapa tu usingizi kwa raha na shida zake. Alikuwa ni mwanamume aliyekuwa amevalia suruali ya rangi ya bluu aina ya Jeans pamoja na fulana ya rangi ya njano iliyochujuka (kaza macho vizuri ndani ya kichaka). Kama alikuwa ni mhalifu aliyekuwa amejificha ndani ya kichaka hiki kwa muda baada ya kufanya uhalifu wake mahali fulani, au ni raia mwema aliyeamua kujipumzisha tu, mimi sijui! Lakini yote kwa yote, mimi na wenzangu kadhaa tuliingia kwenye gari na kuendelea na safari yetu! Usingizi hauna adabu, yakhee! Unakuja tu bila ya wasiwasi mahali popote pale, hata kama ni pa hatari kwa kiasi gani!
No comments:
Post a Comment