Kwa wakazi wa Mji wa Arusha na vitongoji vyake, utaratibu wa watu kujumuika kwa wingi kwa ajili ya kusindikiza maiti, na hasa kuelekea maeneo mbalimbali ya Mkoa wa kilimanjaro, ni wa kawaida tu na umezoeleka sana. Lakini wakati wote katika majumuiko haya, kama wale waliopewa majukumu ya usimamiaji na uongozaji wa masuala kadhaa likiwemo la usafiri siyo waadilifu na hawako makini, basi huwa inageuka kuwa ni kero na usumbufu mkubwa, na hasa pale upendeleo wa wazi wa uswahiba, urafiki na kujuana unapochukua nafasi. Hebu fikiria, kama wewe tangu jana usiku ulikwishaandikisha jina lako kwamba utakuwa ni miongoni mwa wale watakaosafiri kwenda huko anakopelekwa maiti kwa ajili ya maziko; halafu siku ya safari unawahi mapema sana asubuhi katika eneo la kuondokea, lakini eti jina lako linakuwa halionekani kwenye orodha au unaambiwa magari yote hayana tena nafasi (yamekwishajaa)! Lakini wale wanaoonekana kwenye orodha ya asubuhi hiyo, ni wale waliochelewa mno kuandikishwa baada ya wewe kuwa tayari ulikwishaandikishwa! Kisa, eti ni kwa sababu ni maswahiba, ni marafiki na ni watu wanaojuana na msimamizi wa zoezi hilo la uandikishwaji! Kama walikuwa wanajua mapema kwamba watakuwa na watu wao maalumu wanaojuana nao kwa safari hiyo, ni kwa nini wasingewataarifu mapema tu watu wengine ili wasijihangaishe na safari hiyo, ili waendelee na harakati za majukumu yao mengine!
Acheni hizo na hivyo viji-suti suti vyenu!
No comments:
Post a Comment