KWA MROMBOO-ARUSHA; NI MINOFU NA MAPAJA YA MBUZI NA NG'OMBE KWA KWENDA MBELE KILA SIKU...!
Kwa sasa ndilo eneo lililojizolea umaarufu na umashuhuri mkubwa kwa uchomaji wa nyama (nyama choma), kwa wakazi wa Mji wa Arusha na vitongoji vyake pamoja na kwa raia wa mikoa ya jirani, na hasa mkoa wa Manyara (hususan wilaya ya Simanjiro)...
Acha kudondokwa bure na mate, Wakwetu! Fanyafanya maarifa na wewe ufike hapa ujichagulie ya kwako. Bei hapa ni maelewano tu; ni kuanzia Tshs 5,000/- kwa huo mguu mdogo kabisa. Hautoshindwana na muuzaji..
Mpini Wa Shoka ulibahatika kumnasa kijana huyu, mmoja wa wawatayarishaji na wauzaji wa nyama choma katika eneo hili la kwa Mromboo. Anaitwa Habibu Juma, hapa akiwa katika harakati za kuhakikisha nyama za wateja wake zinaiva vizuri na kwa kiwango kinachohitajika... Zikishakuwa tayari, basi hapa kinachobaki ni mwendo wa kachumvi kidogo, kapilipili kidogo... na kalimao kidogo.. Alooo, wewe jamani! Mbona ni uhondo na utamu mtupu! Lakini Mpini Wa Shoka unakutahadharisha sana! Angalia usije ukawa unakuja hapa kila siku, mara kwa mara, kula nyama na marafiki zako, lakini nyumbani kwako watoto wanashindia na kulalia dagaa chukuchuku lisilokuwa na kiungo chochote kile; ni aibu Wakwetu..!
Hizi zote zilizotundikwa na zile zilizo tayari juu ya jiko la moto zinawasubiri wateja; na zinatakiwa zote ziishie matumboni mwa binadamu kwa raha zao...
Wateja kwenye viti na vinywaji vyao mezani wakiisubiri kwa hamu nyama waliyoiagiza iwafikie kutoka jikoni, ikiwa tayari imekwishakatwakatwa vipande vidogovidogo kwa ajili ya kutupia tu mdomoni. Hata kama mfukoni hauna kitu, lakini ukipata nafasi japo kidogo basi Mpini Wa Shoka unakushauri na wewe ujitahidi ufike hapa ili ung'aeng'ae macho na sharubu (ushangaeshange) kidogo, kisha uondoke zako hata na harufu kidogo tu ya nyama choma za hapa kwa Mromboo
No comments:
Post a Comment