ARUSHA-BAADHI YA MITAA NA BARABARA TAYARI!





Kama ukizifuatilia picha nilizokuwekea wakati fulani (waweza kuzitazama chini zaidi), utakumbuka Mpini Wa Shoka ulikuonesha kwa ufasaha jinsi barabara na mitaa kadhaa ya katikati ya Mji wa Arusha ilivyokuwa ikishughulikiwa kwa ukarabati. Sasa, tayari baadhi ya barabara na mitaa hiyo imekwishawekwa lami na imeanza kutumika. Picha ya juu, kama unakumbuka vema kwa picha zilizopita, ni barabara inayopita Msikiti mkuu wa Arusha, ambayo ukiifuata moja kwa moja kama wakina mama hao wawili wanavyoelekea, basi unakwenda kukutana na soko Kuu la Arusha. Na ukiendelea zaidi, unakwenda kukutana na barabara ya OTTU (kwenye picha ya chini), ambayo mbele kidogo inakutana na barabara maarufu ya Sokoine. Mambo katikati ya mji sasa ni raha tupu, japo kero kubwa ni uegeshwaji holela wa magari, unaozifanya baadhi ya barabara na mitaa hii kuonekana ni nyembamba(finyu) mno, na kumbe Wachina wametengeneza kwa upana mzuri tu!

Hapa ni kwenye kamtaa kafupi tu mbele ya jengo la vioo la Salim Alii. Kamtaa haka kafupi kanaunganisha barabara ya Seth Benjamin(kule anakoelekea yule jamaa mwenye shati la rangi nyekundu) na barabara ndefu inayotoka mnara wa mwenge(huku anakokuja huyu bwana kaka mwenye mfuko mweusi mkononi) inayoishia kwenye makutano na barabara ya Sokoine. Kamtaa haka nako lami mpya tayari, lakini kero hapa ni uegeshwaji mlundikano wa magari. Utafikiri ni kajiuchochoro fulani, kumbe ni barabara pana tu!

 

 

    

No comments: