KUWA MAMA WA FAMILIA SIYO KAZI NDOGO.

Wengine wanafikiri kuitwa mama ni kwa sababu tu ya kuzaa watoto. La hasha! Kuitwa mama ni kazi nzito. Sehemu kubwa ya wajibu katika majukumu ya kila siku ya ndani ya familia ni mama ndiye anayeyabeba. Kuhakikisha watoto na familia nzima wamelala usiku salama, na wameamka asubuhi salama. Kuhakikisha wote wanaokwenda shuleni wanawahi kuamka na kuondoka wakiwa kamili kabisa na zana zote kwa mafunzo yao. Kuhakikisha usafi wote wa nyumba pamoja na wa vyombo na nguo za familia yote. Kuhakikisha usafi wa miili ya wanafamilia wote. Kuhakikisha wakati wa mlo unapowadia, basi mlo unakuwa tayari mezani au kwenye jamvi au kwenye mkeka kwa ajili ya familia yake; hiyo ikiwa ni baada ya kuhangaikia kitoweo a.k.a mboga na washirika wake wote (nyanya, vitunguu, mafuta na hata mkaa na kuni, ukiwemo unga wa dona au sembe kwa ajili ya ugali mkubwa). Pamoja na yote hayo, lakini bado wakati mwingine mama huyuhuyu afungue kajibiashara kake kidogo kama kakukaanga fish (samaki), mihogo, viazi, ndizi, vitumbua na mandazi, mama lishe au kuuza matunda na mbogamboga! Huyo ndiye mama wa familia! Siyo mchezo. Mpini Wa Shoka unawapa Big up sana wakina mama wote wanaoziwajibikia na kuzipigania familia zao kwa hali na mali bila ya kuchoka. Siyo wale, kila kukicha ni kiguu na njia kwenda kupiga soga na umbea huku na huko mitaa ya jirani na kujipodoa tu sura!

No comments: