Kama kuna vitu vinavyosifiwa sana kwa utamu, basi miongoni mwao ni asali. Ndio maana hata wakati mwingine utawasikia wapendanao wakiitana majina ya 'asali wangu' ama 'honey', na hasa wakati ule pendo linapokuwa ni la motomoto kwelikweli, kabla halijaanza kuchachuka na kuwa chungu mfano wa shubiri mwitu. Unajua asali inatokana na nini hasa? Hizi ni nyumba za nyuki. Kijiji cha Terrat kipo wilayani Simanjiro mkoani Manyara; Km kama 80 hivi kutoka mji wa Arusha, ambako jana jioni hadi leo mchana, nahodha wako nilikuwa huko nikibarizi kidogo, ndipo nikavutiwa na mtindo huu wa jinsi mizinga hii ya nyuki ilivyotundikwa kwa wingi katika sehemu moja. Inaonekana katika kijiji hiki cha Terrat makundi ya nyuki ni mengi mno, na asali inapatikana kwa wingi! Yaani hapa, maana yake ni kwamba, makazi kwa ajili ya nyuki siyo tatizo hata kidogo. Labda ni hao nyuki tu wenyewe wa kuingia ndio wakosekane!
|
No comments:
Post a Comment