KATA YA DARAJA MBILI, ARUSHA KUMEKUCHA....!

Kufuatia kifo cha aliyekuwa diwani wa kata ya Daraja mbili, jijini Arusha, Marehemu Bashir Msangi (CCM), aliyefariki miezi kadhaa iliyopita, sasa ni wakati wa kuijaza nafasi yake.

Filimbi ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi kwa vyama mbalimbali vya siasa imepulizwa rasmi! Kila chama sasa kazi ni kwake kurusha karata na mitego yake kwa wapiga kura kwa wiki kadhaa ndani ya mitaa na vitongoji vya kata ya Daraja mbili.

Hebu tuzitazame kampeni hizi, Je, zitakuwa ni za kuuza sera na mipango thabiti kwa ajili ya maendeleo ya wana-Daraja mbili, au zitakuwa ni kampeni za kurushiana vijembe, matusi, mambo binafsi, kupondana tu kwa chama kimoja na kingine, na hadithi nyiiiiiiiingi tu jukwaani zisizokuwa na faida wala uhusiano wowote ule na maendeleo ya wana-Daraja mbili? Mpini Wa Shoka kama kawaida kazi yake ni moja tu. Ni kukupa kila ikipatacho. Kazi ni kwako.

 

 

MOTO WA KAMPENI UMEWASHWA....

 

HAPA NI KATIKA MOJA YA MIKUTANO YA KAMPENI YA Chama Cha Demokrasia na Maendeleo-CHADEMA. NI PATASHIKA NGUO KUCHANIKA.....!

 


Mfurukutwa wa chama (shotii) na toy la helkopta mkononi lenye rangi za chama.

 



Maandamano ya nguvu ya kuhamasisha mitaani, kabla ya kuingia kwenye viwanja vya kampeni. 

 

"Chadema! Chadema! Peoples power!" Mwimbishaji jukwaani akionesha umahiri wake wa kuwahamasisha wapiga kura, kabla wageni rasmi na mgombea udiwani kwa tiketi ya chama chao hajafika viwanjani. 

 


Wananchi nao tayari viwanjani wakisubiri kusikiliza sera na mipango ya chama. 



Kwenye mikutano kama hii, kushangaa nako kumo; hata wakati mwingine mtu haeleweki vizuri kama yupo viwanjani kwa ajili ya kusikiliza chama kinasema nini, au naye amekuja na yake mengine tu yaliyomleta ndani ya mkutano!

 

Ni utulivu na umakini wa kutosha. Macho yote yako mbele kumsikiliza aliyepo jukwaani akimwaga mambo yake.

 

Godbless Lema, ambaye ubunge wake kwa jimbo la Arusha ulivuliwa na mahakama, naye akiwa jukwaani kunadi mambo ya chama ndani ya kata ya daraja mbili. Kwa sasa Lema anasubiri kusikilizwa kwa hukumu ya rufani yake ya kuvuliwa ubunge, ambayo imesogezwa mbele.

 

Ni vicheko na raha tupu, wakimsikiliza kwa makini Godbless Lema jukwaani. Kutoka kushoto ni James Millya, aliyekuwa kiongozi wa vijana wa chama cha Mapinduzi-CCM mkoa Arusha, ambaye ni miezi kadhaa tu ya hivi karibuni amehamia CHADEMA, katikati ni mgombea wa nafasi ya udiwani kata ya Daraja mbili, Bwana Msoffe, ambaye katika uchaguzi uliopita uliomweka madarakani diwani aliyefariki, marehemu Bashir Msangi, naye alikuwa ndani ya CCM, na aligombea nafasi hiyo kwa ngazi ya chama na kuangushwa kwa kura na marehemu Bashir Msangi. Aliyeshika tama kama anayeyatafakari maneno ya Lema jukwaani, ni mbunge wa jimbo la Arumeru, mh. Joshua Nasari.    

 

 

No comments: