NI VEMA KUIKUMBUSHA NAFSI YAKO..
Kama kuna jambo ambalo miongoni mwetu tunajitahidi sana kujifanya hatuliwajibikii wala kuzishughulisha saaaaaana nafsi zetu kulikumbuka, ni kifo. Na wengine wanapokuta mahali fulani, hata ndani ya familia zao, kuna mazungumzo yanayohusu suala la kufa, basi hujihisi wazi ndani ya nyoyo zao kwamba hayo siyo mazungumzo mazuri yanayotakiwa. Yabadilishwe haraka! Utasikia, "Aaah! Sasa hayo ni mazungumzo gani tena mnaleta hapa! Nani anataka mambo ya kufakufa hapa!" Na hata wapo wanaodiriki kuwapotosha na kuwadanganya kiimani ndugu, jamaa, marafiki na hata waumini wenzao kwamba kifo hakina uhusiano wowote ule na Mungu! Eti kifo kinatokana na shetani! Kama kweli kifo ni cha shetani, basi kwa maana hiyo ni kwamba shetani ana nguvu kuliko hata Mungu mwenyewe aliyemuumba huyo shetani, kwa sababu hata manabii na mitume wote kama Daudi, Mussa, Nuhu, Ibrahim na wengineo wengi waliotumwa na Mungu hapa duniani, nao pia walikufa! Ndugu yangu usidanganyike. Imeandikwa waziwazi, na kamwe haitogeuka, "kwa hakika kila nafsi iliyoumbwa, ni lazima itaonja umauti." Wewe chacharika na kuhangaika vilivyo huku na huko ndani ya dunia hii kwa kadiri unavyoweza na mipango na dili zako, lakini mwisho wa yote hayo usisahau kwamba sekunde yako ikifika, ni lazima utazimika tu! Wewe unajifanya hautaki kukikumbuka wala kukizungumza kabisa kifo, lakini kumbe kifo chenyewe kinatukumbuka vema na kinatuwajibikia vilivyo. Ndio maana kila sekunde tunavunwa tu!
HAPA ni katika mazishi ya hivi karibuni tu ya mjomba wa mke wangu, marehemu Hamad Saidi Tilya, aliyefariki Majengo ya Juu-Mjini Arusha.... Mwenyeezi Mungu amfanyie wepesi, na amsamehe yale yote aliyokosea hapa duniani.
Makaburi ya Ngaramtoni ya chini-Arusha ambako ndiko mazishi haya yalikofanyikia.
Mwili ukipelekwa makaburini baada ya kufanyiwa ibada.
Kaburi likiwa tayari limekwishachimbwa pembeni mwa makaburi mengine.
Mwili ukishushwa kaburini.
Mwili ukianza kufunikwa kwa udongo. "Tuliumbwa kwa udongo, na tutarudi ndani ya udongo."
Udongo umeshajaa kabisa kaburini.
Kaburi linanyooshwa vizuri.
Haya ni miongoni mwa maagano ya mwishomwisho kwa kulimwagia maji kaburi baada ya dua na maombi kukamilika, kabla ya watu hawajaondoka na kumwacha marehemu pekee yake ndani ya kaburi lake.
Aliyelala hapa yeye siyo mjinga aliyekubali kufa; na wala wewe ambaye bado uko hai ukipumua kwa raha zako siyo mjanja saaaaaaaana kwamba umeweza kujizuia usife. Ni vema kukumbuka kwamba "waliokwishatangulia wao wametangulia tu, na sisi tuliobaki hai ni marehemu watarajiwa ambao nasi pia tumo kwenye njia hiyohiyo waliyoelekea hawa waliolala ndani ya makaburi haya. Ndugu yangu, ikumbuke mwenyewe nafsi yako! Kwenye kaburi utalala peke yako. Haya! Wee shauri yako tu na huu utamu wa hii dunia tunayopita na kuiacha!
No comments:
Post a Comment