HEBU TUENDELEE NA SAFARI YETU YA BARIADI!

....wakwetu, huu unaweza ukawa ni urafiki wa mashaka!

  

Ndani ya Makao Makuu ya Mkoa mpya wa Simiyu; Mjini Bariadi, nilikutana na kihoja hiki. Hebu tazama kwa makini huu urafiki wa Bata na hawa ndege pori. Hawa ndege wakubwa kwa jinsi mimi ninavyowafahamu, mara zote huwa nawaona kwenye hifadhi za mbuga za wanyamapori. Lakini katika Mji wa Bariadi wako kibao kila mahali, nikabaki nashangaa. 

...na urafiki wao na bata katika kujitafutia riziki ndio hasa ulioniacha hoi. Wanakwenda pamoja, hatua kwa hatua!

 

Kweli maisha ni popote, na riziki ni kokote. Si unaona mwenyewe! Ni juhudi tu ya mdomo wako kukifikia kile unachokihitaji!




BARIADI-ARUSHA...!

Siku siyo nyingi sana barabara hii inayoonekana kwenye picha hizi mbili inatarajiwa kuboreshwa kwa kiwango cha lami, ili kuunganisha mkoa wa Simiyu kutokea katika Mji huu wa Bariadi hadi katika mkoa wa Singida hadi Arusha, kwa kupitia wilaya ya Mehatu. Mbona mambo yatakuwa raha tupu. Yaani Arusha-Bariadi itakuwa ni faster tu! 

 

 

                                                         MNADANI!

Katika uzururaji wangu katika Mji huu wa Bariadi, nikafanikiwa kufika katika eneo la Mnada; eneo hili linafahamika kwa jina la Kidinda. Kwa hivyo, mnada huu nao unajulikana kama mnada wa Kidinda. Ni eneo lililopo jirani tu na katikati ya Mji. Ni mnada mkubwa mno, ambao umegawanywa katika maeneo tofauti tofauti kutokana na aina ya bidhaa zinazouzwa. Kuna eneo la mnada wa mazao, eneo la mnada wa mifugo, na kadhalika na kadhalika kwa kadiri ya bidhaa zinazofikishwa katika mnada huu. Lakini Mpini Wa Shoka ulivutiwa zaidi na mnada wa mazao pamoja na ule wa mifugo...

Mnada wa mazao uko mwanzoni kabisa wakati unaingia kwenye eneo hili la Kidinda, ukitokea katikati ya Mji wa Bariadi. Wachuuzi wakiwa kazini. Wanunuzi nao hawako nyuma. Niliulizia bei ya debe moja la mahindi hapa, nikaambiwa ni Tshilingi 12,000/-. Na sadolin (Korondo) ni Tshilingi 3,000/-. Kazi ni kwako. 

 

   

Hapa ni karanga, maharagwe na hata dengu na Choroko.

 


KISHA nikatua kwenye uwanja wa eneo la mnada wa mifugo...

 

Ng'ombe mnadani. Wanunuzi kwa wachuuzi. Wengine wamefika hata na malori na baiskeli kwa ajili ya kukusanya mifugo na kuisafirisha mikoa mingine, na hasa jijini Dar es salaam.

 


Pamoja na biashara ya mifugo, lakini biashara nyinginezo ndogondogo kama za vyakula na vinywaji nazo pia zipo kila upande. Lakini karanga za kukaanga na za kuchemsha nazo pia zipo, kama unavyomwona huyu dogo akiendelea na biznes hiyo. Kwa hali hii, sijui hata kama huyu anaendelea tena na masomo ya shule!

 


Wastani wa bei ya mbuzi hapa ilianzia Tshilingi 40,000/- na kuendelea. Wakwetu, kama unataka kunywa supu, wewe lete tu pesa nikakununulie mmoja fasta.

 Wakati Mpini Wa Shoka ukiendelea na pitapita zake katika mnada huu mkubwa wa mifugo katika eneo hili la Kidinda, ndipo ghafla tu likatokea tukio mmoja la kusikitisha sana. Tukio hili lilianza kama mzahamzaha tu. Lakini ghafla likageuka kuwa balaa. Jamaa mmoja alianza kurushiwa mawe hapa na pale katikati ya umati huu wa watu unaouona, kisha akaanza kuandamwa kwa kufukuzwa kila upande. Polisi-FFU mmoja akafika kumwokoa; akaanza kukimbiana naye akimwondoa katika uwanja huu. Aah! Wapi! Kundi la watu halikuridhika; likaendelea kumwandama tu mtu huyu akiwa na polisi huyu kwa mfululizo wa mawe. Polisi akapasuliwa maeneo kadhaa ya kichwa chake, damu zikaanza kumvuja ovyo. Polisi alipoona mambo yamemzidia; huenda angeweza kuumizwa zaidi au hata kuuawa, akaamua kumwacha yule jamaa akimbie kivyake, yeye akapanda pikipiki ili awahi kupata huduma hospitalini. Wananchi wenye hasira wakaendelea kula sahani mmoja na mtu wao (wakamwandama) huku na kule kwenye mitaa na vichochoro vya eneo hili la Kidinda hadi wakafanikiwa kumnasa; wakampa kipigo cha paka mwizi kwa kila aina ya silaha ya jadi hasa mawe makubwa makubwa hadi wakamuua kabisa! Lilikuwa ni tukio la kutisha kabisa. Gari la Polisi lilipofika katika eneo la tukio, ni kama lililokuwa limekwishachelewa kabisa; wakajibebea tu ndani gari mzoga wa huyo jamaa na kuondoka nao. Hisia zilizokuwepo ni kwamba jamaa alikuwa na mazoea ya kuiba ng'ombe za watu katika maeneo mbalimbali na kwenda kuwauza minadani, ukiwemo huu wa Kidinda. Ndipo safari hii siku zake 40 zikatimia...  

No comments: