HIVI NDIVYO MAISHA YALIVYO.

Kama kuna jambo ambalo kila mtu analitamani sana katika maisha yake, ni kuona anafanikiwa kwa kufikia lengo/malengo ya kile alichokikusudia. Kama ni mwanafunzi wa daraja lolote lile, basi kwake kumaliza masomo kwa alama nzuri ndilo lengo lake. Kama ni mfanyabiashara, kupata faida zaidi na biashara yake kukua kwa kiwango kikubwa ndilo lengo lake. Kama ni mkulima, kuvuna mazao ya kutosha ndilo lengo lake. Kama ni wachumba, siku wanapokamilisha kwa kuoana huwa ni tabasamu tupu. Na kama miaka mingi imepita bila ya kufanikiwa kupata hata mtoto mmoja, siku ujauzito unapokamata; na baadaye mtoto kuzaliwa huwa ni nderemo tupu ndani ya nyumba na simu zitapigwa kila mahali kwa kila mpendwa wao. Na kadhalika... na kadhalika... na kadhalika kwa kadiri wewe utakavyopenda kuyaongeza mengine mengi tu hapa.

 

Pamoja na utitiri huu mkubwa wa malengo ya kila namna, lakini Mpini Wa Shoka unataka uichukue hadithi hii moja tu ya yeyote yule ambaye yumo katika harakati zozote zile za ujenzi wa nyumba yake. Kama kuna zoezi ambalo nimekuja kugundua kwamba linawaumiza mno vichwa watu wengi, basi ni hili la ujenzi. Wakwetu, unaweza ukaanza vizuri msingi, kisha ukaanza kupandisha polepole kwa matofali ya aina yoyote ile, au hata kama ni ya miti, lakini wakati ukiwa unakazana vilivyo, mara ghafla ile shughuli ambayo ndiyo uliyokuwa ukiitegemea kukupa vijisenti vya kuufanyia huo ujenzi wako inaharibika; na hauna tena njia nyingine yoyote ile ya kupata senti mahali popote pale! Unajikuta ukitumbua tu macho kwa uchungu na sononeko! Ni hadithi iliyopo kwenye nyoyo za watu wengi mno......   

Hebu tazama mfano wa nyumba hii. Inawezekana imekuvutia sana kwa mtindo wake unavyoonekana kwa nje. Sasa kwa bahati mbaya mwenye nyumba hii kama chanzo chake cha vijisenti kikikwama tu, huenda jengo hili likabaki vivi hivi kwa miaka mingi tu, na ikimbidi basi ahamie vivyo hivyo! Kwa kweli, ujenzi ni kazi ngumu. Hadi jengo lako likamilike kabisa na wewe kuhamia, ni jambo la kumshukuru mno Mwenyezi Mungu.

   


Hapa ni mchanganyiko mtupu. Mwingine amekwishapaua na kuweka madirisha na milango! Mwingine amepaua tu lakini madirisha na milango bado! Mwingine hata kupaua bado japo amekwishalikamisha kabisa jengo lake kwa matofali! Na mwingine huenda ndiye aliyekuwa wa kwanza kabisa kuanza kujenga katika eneo hili kabla ya jengo jingine lolote hapa, lakini sasa yeye ndiye anayeonekana wa mwisho kabisa baada mambo ya vijisenti kumharibikia ghafla tu, na jengo lake limebakia limedoda tu hata miti na mapori yameanza kuota ndani yake na kufuga majoka na vyura!  Na wakati mwingine hata lijiangukie tu kutokana na miaka mingi kupita bila ya kuendelezwa wala kushughulikiwa tena! Masikini!

 

Ama, Kweli, Kwa malengo yetu ya kila namna tuliyonayo, basi ni vema tumwombe mno Mwenyezi Mungu atusaidie ili tuweze kuyafikia na kuyafanikisha katika mwaka huu mpya wa 2013. 

 

No comments: