Ndugu, Jamaa na Marafiki, kumbukeni kutembeleana. Siyo hadi zifike zile siku za misiba na sherehe tu...
Leo nilipata bahati ya kutembelea katika eneo linalofahamika kama Olosiva lililopo katika kata ya Kiranyi; Arusha vijijini. Nilishiriki katika kuwatembelea ndugu na jamaa waishio katika eneo hili. Siyo eneo ambalo lipo kilometa nyingi sana kutoka katikati ya jiji la Arusha. Ni eneo lililopo juu mlimani. Kama unatokea Arusha Mjini na unaelekea Mji wa Ngaramtoni kwa barabara ya Arusha-Namanga, basi ukifika katika eneo maarufu linalofahamika kwa jina la Kwa Iddi, hapo muulize mtu yeyote yule atakuonesha bila ya wasiwasi barabara zinazoelekea Olosiva....
Na hii ndio nyumba hasa tuliyokwenda kuitembelea hapa Olosiva. Ni nyumbani kwa Bi Khadija Jamma, ambaye kwa wenyeji wa hapa Olosiva anafahamika zaidi kama mama Faiz.
Mazungumzo marefu ya hapa na pale ya kuimarisha udugu baina ya wanandugu yakapita kwa vicheko, bashasha na tabasamu za kutosha, na kisha Mpini Wa Shoka kama kawaida ukawanasa katika picha ya pamoja....
Picha zote mbili; waliokaa nyuma kutoka kushoto ni Bi Amina Ally (mama Ibra au mama Halima, mwalimu) mkazi wa Sanawari, Bi Khadija Saidi Kivuyo (mama Abdillahi, mama kilimo) mkazi wa Njiro na Bi Fatuma Jamma (mama Kimala) mkazi wa Saitabau (ni jina tu la eneo, japo kwa kawaida ni jina la mtu). Na waliokaa mbele kutoka kushoto ni Bwana Abdillahi Mohamed Laizer (Anko, babu Abdillahi) mkazi wa Olosiva na mwenyeji wao (mwenye nyumba) Bi Khadija Jamma (mama Faiz). Ni tabasamu na cheko tu za pamoja za wanandugu hawa kukutana pamoja.
Kwa hakika ni vema sana kutembeleana kwa wanandugu kama hivi. Siyo habari ya kusikia tu kwa masikio kwamba ndugu yako fulani anaishi sehemu fulani katika Mji huohuo unakoishi wewe, lakini hata siku moja haujawahi kwenda kumtembelea, na wala haujui kabisa anaishije! Na wewe je, una mpango gani wa kumtembelea nduguyo, jamaa yako au rafikio, hata kama mambo yake ya kimaisha siyo safi saaaaaaaaaaaaana! Nenda ukamwone.
Baada ya hapo, kabla ya kuondoka katika eneo hili la Olosiva, Mpini Wa Shoka ukaamua uyatazame mandhari yake.....
Eti, wenyewe wakazi wa hapa wanajiita wanaishi kijijini! Kwa macho yako na wewe, unakubaliana na hilo kwamba hapa ni kijijini?
Na mojawapo ya vitu vilivyonivutia sana wakati nikiwa hapa Olosiva, ni jinsi unavyouona kwa mbali mno Mji maarufu wa Kwa Mromboo uliopo kilometa kadhaa kutoka katikati ya Jiji la Arusha kwa barabara kuu ya Arusha-Simanjiro-Kiteto
Hivyo unavyoviona vyeupevyeupe kwa mbali, ni mabati (mapaa) ya nyumba katika Mji huo wa Kwa Mromboo. Kwa hakika, kwa kutokea hapa Olosiva, Mji wa Kwa Mromboo uko mbali kwelikweli!
No comments:
Post a Comment