WAKWETU, HIZI NILIZISAHAU TU!
Wakati nilipokuwa narejea kutoka safari yangu ya Kanda ya Ziwa kwa kupitia njia ya Musoma-Serengeti-Ngorongoro-Arusha, Wakwetu pia niliokota mbili tatu njiani. Hata sielewi nilizisahauje hizi kukurushia mapema. Lakini poa moyo....pamoja sana.
Hiki ndicho chombo nilichosafiria kwa safari hii nikirejea Arusha. Chombo kimetulia kwelikweli hiki. Kitu CoastLine, Wakwetu. Yaani kwenye barabara ya vumbi utadhani uko kwenye lami!
Asubuhi na mapema, kijua ndiyo kwanza kinaanza kuchomoza kwa mbaaaaaaaaaali!
Hili ni bwawa kubwa linalotegemewa zaidi na wakazi wa Mji wa Butiama (Mji alikozaliwa Rais wa kwanza wa Tanzania, marehemu mwl Julius Kambarage Nyerere) na vitongoji vyake pamoja na vijiji kadhaa vya maeneo ya Musoma vijijini kwa huduma ya maji kwa matumizi ya majumbani, na hata kwa kilimo cha umwagiliaji. Humu pia samaki wamo kibao tu; wavuvi huwa wanapiga makasia kama kawaida ili kujitafutia kitoweo cha nyumbani na cha biashara. Wakwetu, hapa tulipita asubuhi sana; na hata picha hii niliipiga kwa bahati tu wakati nimeshituka ghafla usingizini. Si unaelewa tena safari za kuanza alfajiri huku ukiwa bado una usingizi mwingi kichwani!
VIBOKO!
Kama kuna jambo ambalo mara zote ninapopita katika mbuga ya Serengeti huwa linalivutia sana, basi huwa ni kijisehemu hiki kidogo ambacho kwa mwaka mzima huwa kimejaa maji tu na utayaona makundi ya viboko yakiwa yamejilaza kwa utulivu mfano wa mawe makubwa. Eneo hili liko jirani tu na Seronera ndani ya Serengeti. Siku moja nitataka kujua vema ni kwa vipi kibwawa hiki kidogo cha viboko huwa hakikauki maji kwa karibu kipindi chote cha mwaka!
No comments:
Post a Comment