MAMBO YA MVUA HAYA!
Katika maeneo mengi ya mikoa karibu yote nchini Tanzania, kwa sasa mvua zinanyesha kwelikweli. Kwa wakulima na wafugaji vijijini na mashambani, kwa kweli kwao ni raha na furaha tupu. Lakini kwa watu wengi wa maeneo ya mijini, mvua kwao huwa ni kitu kinachowanyima kabisa raha; japo ndani ya nyoyo zao nao wakati fulani huwa wanaitamani sana ili iwaondolee vumbi mitaani pamoja na joto lililokithiri ndani ya vyumba vya nyumba zao! Wakwetu, Ama, kweli, kama Mwenyezi Mungu angeamua kuleta (kunyeshesha) mvua kwa kufuata matakwa na ratiba za jinsi vile ambavyo wanadamu wenyewe wangelitaka, basi nina uhakika mkubwa kwamba huenda maeneo mengi ya mijini mvua ingelikuwa inanyesha kwa nadra sana! Si haitakiwi kwa wingi saaaaaaaaaaaaana! Inatakiwa iwe kiduchu (kidogo) tu!
Hapa ni Arusha mjini leo adhuhuri (mchana). Mvua kubwa ilianza kutandika kwa nguvu, kila mahali ikawa ni hekaheka na mshikemshike mtupu kwa wakazi wake. Mimi mvua hii ilininasia nikiwa maeneo haya unayoyaona hapa chini. Ni maeneo ya Florida, jirani na chuo cha mafunzo ya ufundi-Arusha (Arusha Technical College). Burudani kubwa hapa ikawa ni miamvuli kila mahali kwa watembeao kwa miguu....
Hata wenye huduma ya usafiri wa pikipiki (bodaboda), iliwabidi nao wajitahidi kuwahifadhi wateja wao ili wasilowane sana.
Ni heri baba alowane, kuliko kitoto kichanga mgongoni...
Kumbe mvua ikikolea vizuri, lifti ya Mwamvuli nayo huwa inakubalika tu sawa na ile ya gari au ya baiskeli!
Hakuna pa kuikwepea, Wakwetu! Ni mvua tu kila upande.
BARABARANI KWA WAENDESHAO VYOMBO VYA MOTO NAKO......
Ilikuwa ni hatari tupu. Mvua ilisababisha hata madereva wasiweze kuona vema mbele na nyuma kwa kupitia kwenye vioo vyote vya magari yao! Umakini, uangalifu na utulivu wa ziada ndio uliomsaidia kila mmojawao hapa. Na kwa sehemu kubwa, magari mengi yaliendeshwa huku yakiwa yamewashwa taa zote, ili kuepusha kutokea kwa ajali. Hapa ni kwenye mataa ya kuongozea magari (traffic lights) eneo la Mianzini mjini Arusha. Dalala na magari mengine unayoyaona hapa, ni kwenye barabara ya Florida yakielekea kukamata njia ya kwenda Moshi (mkoa wa Kilimanjaro), Dar hata Tanga kama yakikata mkono wa kulia. Na yale yanayokwenda kukata mkono wa kushoto, ni yale yanayoelekea kwenye barabara ya Arusha-Namanga-Nairobi-Kampala.
No comments:
Post a Comment