HALI YA HEWA YA MJI WA ARUSHA KWA SASA AIHITAJI KUIFANYIA MZAA HATA KIDOGO, WAKWETU...!



Kwa kawaida, kila unapoanza kuingia msimu wa mwezi wa 6 wa kila mwaka, Mji wa Arusha huwa unaingia katika kipindi cha kutawaliwa na hali ya hewa ya baridi (na wakati mwingine ni baridi kali mno). Hali hii huendelea hadi kufikia mwezi wa 8, ndipo huanza kupungua taratibu. Katika kipindi chote cha hali ya baridi, ni vema sana kwa kila mkazi wa Mji wa Arusha na Wilaya zake zote, na hata kwa wakazi wa Mkoa jirani wa Manyara, kuchukua tahadhari na uangalifu wa makusudi kabisa juu ya kuikinga miili yao dhidi ya hali hii ya ubaridi. Na hasa wale wenye watoto wadogo, ndio hasa wanaohitajika kuwa makini kabisa katika kuhakikisha watoto wao wanavuka salama katika kipindi hiki. Vinginevyo, ni vema ukatambua kwamba endapo ugonjwa wa nimonia unaosababishwa na baridi ukifanikiwa kuingia mwilini, basi ujue kabisa kwamba gharama ya kuutoa hospitalini ni kubwa, na muda wako mwingi kwa ajili ya harakati na pilikapilika zako mbalimbali hasa za kikazi utapotea bure. Wakwetu, baridi haina cha  umwamba, ujasiri wala ushujaa. Ni vema ukachukua tahadhari zote zinazofaa. Kinga ni bora kuliko tiba...

   

Unapoingia kitandani kulala, blanketi zito mfano wa hili ni muhimu mno kwa mwili wako na hata kwa watoto wadogo...

 

 

 

Nyakati za asubuhi na zile za jioni na usiku, masweta na makoti kama haya ndizo silaha thabiti kwa mwili wako. Habari ya mashati yako mazuri unayoyapenda sana iweke mbali kabisa na akili yako, hadi kipindi hiki kitakapomalizika.




Soksi nzito kama hizi ndizo zinazofaa kuvaa miguuni wakati wote, hata usiku wakati wa kulala. Siasa ya kuvaa soksi nyepesi pamoja na viatu vya wazi (makobaz), kwa kipindi hiki haina nafasi hata chembe. Ukilazimisha, ujue ni wewe mwenyewe ndiye unayejiweka hatarini 





Asubuhi na jioni hadi usiku, kofia kama hizi (maarufu kwa jina la boshori) ndizo mwafaka kuvaa kichwani ili kupata joto la kutosha.

 

 


Kama unaweza kupata soksi za mikononi mfano wa hizi, napo pia ni vema kwa kukabiliana na baridi, na hasa katika zile siku ambazo baridi huwa ni kali sana

 

 

 

Vivazi kama hivi kwa kipindi hiki, kwa kweli havina nafasi kabisa ndani ya Mji wa Arusha. Labda ukivalie kwa ndani ya mavazi mengine mazito utakayoyavaa.

No comments: