MACHIMBO YA MCHANGA; MIRONGOINE-ARUSHA


Kama Machimbo haya yangekuwa ni ya madini ya dhahabu, almasi au hata Tanzanite, basi huenda yangekuwa ni miongoni mwa machimbo ya aina yake, kwa sababu pasingekuwa na msimu maalumu wa kupata mawe ya madini! Mawe yangelikuwapo tu kwa kipindi chote cha mwaka mzima. Machimbo haya maarufu ya mchanga ya Mirongoine ndiyo yanayoujenga kwa kasi, usiku na mchana, Mji wa Arusha. Yapo kwenye kijiji cha Mirongoine-Arusha vijijini, wastani wa kilometa 37 kutoka katikati ya Mji wa Arusha kwa kupitia barabara kuu ya Arusha-Simanjiro-Kiteto. Ni miaka nenda-rudi tangu miaka ya 80 machimbo haya yalipoanza kupata umaarufu, na hatimaye kushika kasi kubwa kuanzia miaka ya 90, yameendelea kuwa sehemu muhimu mno kwa ujenzi wa Jiji la Arusha, ambalo kwa sasa linakuwa kwa kasi kubwa. Hakuna mwaka ambao palisemekana machimbo haya yamekuwa na uhaba wa mchanga. Yaani kadiri wachimbaji wanavyochimba na kuusafirisha, basi msimu wa mvua unapofika maji ya mto (korongo kubwa) yanaurejesha tena mchanga katika kiwango chake kilekile! Ama, kweli, mwache Mungu aitwe Mungu kwa maajabu ya uumbaji wake wa ajabu kama huu...



Unauona mchanga ulivyojaa vilivyo korongoni? Unasubiri tu kubebwa ili ukafanye kazi ya kujengewa



Mandhari ya mto (korongo)




Mojawapo ya magari yaliyonaswa na Mpini Wa Shoka yakipakizwa mchanga ndani ya mto (korongo). Kuna ushuru unaolipwa kwa Serikali ya Kijiji cha Mirongoine kutoka kwa wenye magari wanaokwenda kuchukua mchanga. Na pia katika kijiji hiki kuna idadi kubwa ya vijana waliojiajiri wenyewe kwa ajili ya kazi ya kupakiza mchanga kwenye magari, kwa hivyo nao pia wanalipwa. Si unawaona mwenyewe jinsi wanavyochacharika na kushughulika vilivyo? Kwa taarifa yako, hiki kigari ni kidogo sana. Hapa huwa yanafika hata magari ya tani 10 na zaidi, na vijana hawa huwa wanayajaza tu mchanga kama kawaida!

No comments: