KUUELEKEA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI-JULY'2013...


Waislamu katika maeneo mbalimbali ya nchi ya Tanzania na ukanda mzima wa nchi za Afrika Mashariki, Kusini na Kati mwishoni mwa mwezi wa 6 hadi kuingia mwanzoni mwa mwezi wa 7, wamekuwa katika hekaheka na harakati nyingi za kufunga shule za watoto wao kwa elimu ya dini (madrasa) pamoja na kufanya maadhimisho ya kuzaliwa kwa mtume Muhammad (S.A.W). Na isitoshe, ndani ya tarehe hizi pia pamekuwepo na harakati nyingi za shughuli za harusi hapa na pale. Mpini Wa Shoka umebahatika kualikwa na kuhudhuria kona mbalimbali, na hasa katika Jiji la Arusha. Na hii ni mojawapo ya shughuli za ufungaji wa Madrasa pamoja na maadhimisho ya mtume Muhammad (S.A.W), zilizofanyika katika uwanja wa Msikiti wa Tawba (Masjid Tawba) uliopo eneo la Tanesco-Njiro, ambapo kwenye msikiti huu kuna madrasa yao iitwayo Al Rahman (Al Madrasat Rahman). Mambo yalikuwa mengi mno, lakini hebu na wewe shiriki japo kwa uchache tu....


Huu ndio Msikiti wenyewe wa Tawba (Al Masjid Tawba)



Mandhari ya uwanja nje ya Msikiti ilivyopambwa vema, pamoja na umati mkubwa wa waliohudhuria....




Umati wa waliohudhuria, wake kwa waume...




Mwanafunzi wa Al Madrasat Rahman, Hafsa Nassoro akiwa mbele ya hadhara akionesha jinsi alivyohifadhi Quran kwa kuelezea jinsi wingi wa makosa ya binadamu unavyosababiswa na ulimi... 




Karim Salimu yeye akielezea jinsi ilivyo vibaya kuwaudhi wazazi wawili (waliokuzaa)




Faidha Mustafa akisisitiza umuhimu na faida ya kuswali na kuzitimiza vema na kwa wakati sala tano kwa kila siku iendayo kwa Mwenyezi Mungu kwa kila mwislamu...




Wakina mama wakifuatilia kwa makini wakati watoto wa Al Madrasat Rahman wakiendelea kuonesha uwezo wao wa kuhifadhi Quran na kuelezea mambo mbalimbali ya kidini...




Mgeni rasmi wa shughuli hii, sheikh Kisiwa, naye akitoa neno. Na alichokisisitiza zaidi, pamoja na kujiweka sawa kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, lakini umuhimu wa kuuliza na kujifunza kutoka kwa wale wenye elimu, ili kujiepusha na kufanya mambo ya kidini kwa makosa...




Abass Khalfani akielezea habari za kifo..




Sumaiyah Sadik yeye akizungumza juu ya siku ya kiama (siku ya malipo mbele za Mwenyezi Mungu). Nyuma yake wanaonekana waongozaji wa shughuli hii (walimu wa madrasa), ustaadh Suleimani Ramadhani (mwenye kofia nyeupe) na ustaadh Twaha Mohammed.




Mmoja wa akina mama maarufu wa Njiro (mkazi wa eneo la Njiro-Tsunami), Bi. Zulfa Mhina 'Mama Abuu' akiwa na binti yake, Mariam Sadik (aliyeweka mkono shavuni), wakifuatilia kwa makini mambo yote yanayoendelea. Mama huyu ambaye pia ndiye mama mzazi wa mtangazaji wa Redio One ya jijini Dar es Salaam, Aboubakar Sadik, amekuwa ni miongoni mwa akina mama wa eneo la Njiro wenye kufanya juhudi kubwa za kuhakikisha watoto wadogo wa kiislamu wanapata elimu ya dini kwa kuwatafutia walimu wa kuwafundisha, na hata kujitolea eneo la nyumbani kwake kutumika kwa kazi hiyo. Na pia ameanzisha na kuendesha kituo cha elimu ya kawaida ya awali kwa watoto wadogo (chekechea)-kilichopo Njiro-Tsunami, Kiitwacho Sal Star.   




Wengine walikuwa wamesimama kandokando. Kazi yao kubwa ilikuwa ni kusaidia kazi hapa na pale na kuwaelekeza wageni waliokuwa wakifika au kuhitaji huduma yoyote ile. Aliyevaa kofia ni Bwana Nuru Omari Madai na mwenzake Ayub Rashid.




Kila palipo na wazee, basi ujue wazi huwa hapaharibiki jambo kirahisi. Wazee hawa nao pia walihudhuria. Kutoka kushoto ni Mzee Ahmed Mavura, Mzee Bakari, Mzee Mussa na Mzee Hassan




Kutoka kushoto ni Bwana Almasi-mwalimu wa Chuo cha uhasibu Arusha, Bwana Munisi Min-Haji, na Ahmed Mavura.



 

 Kama kawaida! 'Majembe' ya kazi hayakukosekana katika shughuli hii; nayo pia yalikuwepo ya kutosha. Hebu tazama vimbwanga vyao...

 





Wengine walipenda hata Mpini Wa Shoka uwaweke kwenye picha ya pamoja. Kutoka kushoto: Mdogo kabisa aliyeachia tabasamu la maana ni Sumaiyah Jigge, Shadya Jigge, Tahir Athumani Sadik na Bwana mkubwa Anko Saadi Abdillahi Chembe. Wote wakazi wa Njiro





MASHINDANO YA KUHIFADHI QURAN, NAYO PIA YALIFANYIKA..



Hii ndio meza ya majaji (mahakimu) wa usomaji wa Quran




Mmoja wa washindi wa juu kabisa wa usomaji wa Qurani (kuhifadhi), Naima Hamdani, baada ya kutangazwa na majaji...





Mshindi mwingine, kijana Ayoub Khalid akionesha bahasha yake aliyokabidhiwa yenye 'kitu kidogo





Hawa ni washindi kwa upande wa vijana wakubwa. Mwenye kilemba chekundu ni Rashid Omari, Mohamed Aziz (katikati) na Jumanne Rashid.



Familia ya Mpini Wa Shoka nayo pia ilikuwepo. Bibie Khadija Abdallah Chembe aliyembeba mwanawe, Shadya Jigge, akiwa na wifi yake, Bi. Mariam 'Mama Saad' anayeshughulika na simu mkononi.  




Shughuli ilikuwa imesheheni ubora kwa kila idara...Na hapa unapaonaje, Wakwetu? 

Hata kama haujui kusoma wala kuandika, lakini hata kwa hizi picha tu si umeelewa vema! Au unataka pia uelezewe hiki ni nini! Acha utani wewe! Ni Uhondo wa shughuli huu...




Vijana wa Madrasa kutoka eneo la Ngarenaro-Arusha, nao pia walikuwa ni miongoni mwa madrasa kadhaa za Mji wa Arusha zilizoalikwa ili kuwapa nguvu wenzao wa Al Madrasat Rahman katika shughuli yao hii ya kufunga madrasa yao. Hapa wakifanya kweli katika mojawapo ya Qaswida zao tamu iliyowasisimua wengi. 

 

"Mpini Wa Shoka unakutakia wewe mwislamu kote duniani heri ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Mwogope mno yule aliyekuumba, ili ufunge kwa dhati. Na wala usiwaogope wanadamu wenzio, ukafunga kinafiki. Hatari"

No comments: