MFEREJI UMETENGENEZWA VEMA NA WACHINA, LAKINI...!


Mfereji huu kabla ya kutengenezwa na wachina na kuwa hivi unavyouona, ulikuwa ni mfereji fulani mchafu kwelikweli ukitokea eneo la Majani ya Chai ukiambaamba pembezoni mwa ukuta wa shule ya Sekondari ya Arusha (Arusha Sec) na kiwanja cha N.M.C-National Milling Co-operation (kwa sasa soko la wachuuzi wadogowadogo), na kuja hadi hapa kwenye eneo hili la Relini; jirani kabisa na Kituo cha kulelea watoto watukutu, maarufu kama jela ya watoto (kwenye majengo meupe wanakoelekea watu). Kwa sasa baada ya kuboreshwa na wachina, mfereji huu umeongezewa majukumu, ambapo umeunganishwa na mfereji mkubwa uliojengwa kutokea Soko Kuu la Arusha katika eneo ambalo limekuwa ni sugu kwa kutuamisha maji katika kipindi cha mvua; maji ambayo kiasili huwa yanatokea kwenye maeneo ya viinuko vya Mlima Meru, na hasa pande za Sanawari na Mianzini....   





Sasa maji yote yanapofika katika eneo la Relini, yanavuka upande wa pili kwa kupitia kwenye makaravati haya ambayo pia wachina wameyaimarisha zaidi kwa kuyajengea vema kama unavyoyaona, kwa kuhofia kwamba katika kipindi cha mvua huenda wingi wa maji utaweza kuyasomba makaravati haya na kusababisha uharibifu wa Reli. Ni kweli wachina wamefanya kazi yao vizuri na kitaalamu sana, lakini sasa tatizo na hofu kubwa ipo kwa wakazi wa Kata ya Daraja mbili ambako maji ya mfereji huu yanakwenda kupita. Kabla mfereji huu haujaboreshwa kwa kiwango hiki unachokiona, mfereji huu ulikuwa ukileta kizaazaa kikubwa nyakati za mvua kwa wakazi wa Kata ya Daraja Mbili katika eneo maarufu linalofahamika kama kwa Kiboko (Bongonyo Street), ambapo mafuriko yake huwaletea wakazi wake usumbufu na uharibifu pamoja na upotevu mkubwa wa mali zao. Sasa swali la Mpini Wa Shoka ni hili: "Kama wakati ule kabla haujaboreshwa na kuunganishwa na mfereji mkubwa kutoka Soko Kuu ulikuwa ukiwatesa wakazi hao wa Kata ya Daraja Mbili (Kwa Kiboko), je kwa kipindi hiki ambapo umeboreshwa itakuwaje kwa wakazi hao mara mvua zitakapoanza kunyesha?" 

Ni Majanga na mabalaa matupu. Tahadhari ni bora, kabla ya hatari.   

No comments: