TAMU NA CHUNGU YA SAFARI; MPINI WA SHOKA NA VIJANA WAKE WAIONJA KASHESHE YA KUHARIBIKIWA NA CHOMBO MBUGANI...


Tuliamua tusafiri kidogo tutoke nje ya Mji. Tukaamua kuondoka kuelekea Mirongoine (mwendo wa kama km 40 hivi na ushehe kutoka Arusha Mjini) kule kwenye machimbo ya mchanga usiokwisha ili na sisi tukabebe wenyewe huo mchanga na kuuleta Arusha Town. Mpini Wa Shoka ndio uliokuwa kwenye usukani ukipiga gia...



Baada ya kutoka katikati ya Mji; safari yetu ilianzia rasmi kwenye Mji wa Kwa Mromboo. Hapa Mpini Wa Shoka (kofia nyeusi kichwani na sweta la bluu) na swahiba wake, Daudi Mapande a.k.a Makingo wakijaribu kumsaidia bibi mmoja aliyeomba usafiri wa kuelekea kwenye vijiji vya huko kwenye machimbo ya mchanga tulikokuwa tukielekea...




 

Safari yetu ilikuwa murua kwelikweli, lakini ghafla tu...!

 

Wakati tukiwa tumekaribia kabisa kufika kwenye Kijiji cha Ujamaa tukitokea Kijiji cha Mirongoine (wastani wa kama km 3 au 4 hivi baina ya vijiji hivi viwili) tukawa tumeipoteza kidogo barabara sahihi tuliyokuwa tukiihitaji. Mambo ya porini kwenye barabara za vumbi barabara zisizo rasmi huwa ni nyingi mno kupitiliza, bila ya mpangilio maalumu. Wakati tukifanya juhudi za kurejea kwenye barabara sahihi, mara ghafla gari likajikita kwenye sehemu ngumu ya udongo wa barabara, rejeta ikapata mshituko kidogo na feni ikasimama kuzunguka. Hapo ndipo tamu na chungu ya safari yetu ikaanzia. Ikawa si safari tena, bali ni kasheshe tupu..  




Wanaume tukaamua tupambane ili tuweze kurejea na chombo chetu Arusha mjini. Swahiba Rashid Hemedi Charema 'Shidi' (mwenye shati jeusi) akiwa na swahiba wake, mwalimu wa shule ya msingi Themi-Arusha (mwenye shati jeupe) ambaye naye aliamua kuungana nasi katika safari hii ili kwenda kuyaona machimbo ya mchanga ambayo yeye alikuwa hajawahi kuyatembelea. Aliyekaa chini akijiandaa kuingia chini ya uvungu wa gari ni kijana Yusuph (mwenyeji wa Kijiji cha Ujamaa) aliyefika kutusaidia. Pembeni linaonekana lori kubwa likiwa limeshibishwa vema shehena ya mchanga tayari kwa kuelekea Arusha Town




Hii ndio mbuga ya Kijiji cha Ujamaa. Eneo lote ni mchanga mtupu 





Gari limeshiba mzigo wa mchanga tukirejea Arusha Town, lakini mwendo wetu ulikuwa ni sawa na wa konokono; kila mara ilitulazimu kusimama na kukaguakagua na kuongeza maji. Mpini Wa Shoka ukimtazama kwa makini swahiba, Daudi Mapande a.k.a Makingo aliyeinama akichungulia chini..





Hii ndio ikawa kazi yetu kubwa wakati wote wa safari. Safari ya wastani wa mwendo wa saa moja labda na nusu hivi kati ya Kijiji cha Ujamaa hadi Arusha Town, ikatuchukua kuanzia saa nane ya mchana hadi saa 4 ya usiku. Hata hivyo tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu tulifanikiwa kufika salama, japo tulikuwa hoi bin taabani. Hapa swahiba Rashid Hemedi Charema 'Shidi' (anayetazama kamera) na swahiba wake, mwalimu wa shule ya msingi Themi-Arusha (mwenye shati jeupe) wakiwa pembeni mwa swahiba Daudi Mapande a.k.a Makingo anayeongeza maji kwa ndoo

No comments: