MAJINA YA MABASI!

Wakati wa safari yangu ya Dar-Mtwara-Dar, pamoja na mambo mengi ambayo Mpini Wa Shoka umekuwa ukikutupia, lakini hili nalo lilinivutia sana. Sehemu kubwa ya majina ya mabasi yanayokwenda (yanayopita) njia hii yalinipa burudani ya aina yake moyoni. Kama ningeliyaandika tu majina haya bila ya kukuonesha kwa picha, basi nina uhakika ungeweza kuhisi labda Mpini Wa Shoka umeongezea chumvi na kachumbari zake tu za kizushi! Lakini wapi, wakwetu! Hebu soma mwenyewe kwenye haya baadhi tu ya mabasi. Haijalishi ni la safari ya Dar-Lindi-Mtwara..! Dar-Masasi..! Dar-Nachingwea..! Au kwingineko kokote kule katika mikoa hii ya Kusini.... 

Hili Linaitwa Somea. Sasa sijui linakuhimiza usomee kitu gani hasa!


 Hili linaitwa Wifi. Sasa sijui ni wifi yake nani! Na mimi nikianzisha basi langu nitaliita Shemeji Au Shangazi. Unaonaje hiyo!





Hili linaitwa Karafuu. Sijui ni karafu za Zenji (Zanzibar), au ni za wapi yakhe! Mimi basi langu nitalipa jina la Kitunguu Trans Au Ngogwe Trans (Nyanya chungu). 

 


 Hili linaitwa Mkuu. Sasa sijui ni Mkuu wa Meza..! Mkuu wa Majeshi..! Mkuu wa nchi..! Au mwenye basi hili asilia yake hasa ni kutoka eneo la Mkuu-wilaya ya Rombo, mkoa wa Kilimanjaro! 


 Hili linaitwa Najma (soma ubavuni). Yawezekana ni jina la binti wa mwenye basi, Au ni la mke wake mdogo, kipenzi cha roho!


 Hili linaitwa Siri Yako. Sijui hata ni siri ya kitu gani iliyomo ndani ya basi hili!



Hapa ni Swahili. Ndani ya hili basi yawezekana ni marufuku kuzungumza lugha nyingine yoyote ile. Ni Kiswahili tu pekee ndicho kinachoruhusiwa. Haiwezekani! Je kama Wakorea, Wachechnya, Waalbania na Waturuki wasiojua kabisa kiswahili wakitaka kusafiri na basi hili, ina maana itawabidi wao wawe kama mabubu tu mwanzo wa safari hadi Mwisho!

 



Wakwetu, haya ni baadhi tu ya majina ya mabasi ya njia (barabara) hii. Lakini pia lipo basi linaitwa Buti la Zungu! Na Daladala moja reeeefu nililifuma maeneo ya Mbagala rangi tatu jijini Dar es salaam linaitwa Shilingi. Lakini kwa sababu ya mwendo kasi, Mpini Wa Shoka ulishindwa kuyanasa kwa haraka.

  

No comments: