SAFARINI; DAR-MTWARA-DAR

Wakati wa safari yangu ya Dar-Mtwara-Dar, kwakweli niliinjoi ile kisawasawa. Hebu pitisha jicho taratibu uuone Mpini Wa Shoka ulivyosafiri....

Hiki ni miongoni mwa vyombo nilivyosafiria. kinaitwa Maning Nice. Hapa tumesimama kidogo safarini kwa ajili ya kuchimba dawa (kujisaidia), na kula mahindi na karanga hapa na pale. Kama tumbo lako ni sawa na la kwangu, basi usijaribu kuwa na tabia ya kulakula hovyo safarini. Siku moja utakuja kuumbuka, Wakwetu!

 


DARAJA LA MKAPA.

Uwanda wa bonde la Mto Rufiji unavyoonekana vema pembezoni mwa daraja hili. Hapa basi letu lilipita kwa mwendo wa kasi ya ndege.

 

 

Barabara bado iko matengenezoni. Bado haijakamilika. Vifaa vya ujenzi viko kila mahali eneo la barabara, ambalo bado halijawekwa lami; ni kama Km 60 tu. Na hiki ndicho miongoni mwa vitu vinavyowafanya wananchi wa Mtwara wachachamae kwelikweli juu ya suala la gesi iliyogunduliwa mkoani mwao hivi karibuni kwamba, ni kwa vipi mambo ya gesi yanapelekwa harakaharaka na serikali, wakati hii barabara haiishi na miaka inakwenda tu..! Inakwenda tu...!

 


 MVUA ZINANYESHA VILIVYO.....

Mpini Wa Shoka ukiwa ndani ya basi ulijitahidi kukuokotea uhondo na utamu wa barabara ya Dar-Mtwara kwa wakati huu wa kipindi cha mvua katika kipande ambacho bado hakijakamilika. Ni raha na karaha tupu. Sehemu yote ni urojo mtupu!

 



Uharibifu wa mazingira nao hauko nyuma, japo bado kuna maeneo mengi yenye misitu mikubwa....

Magunia ya mkaa barabarani yanasubiri wateja, hasa wale wenye malori na mabasi.






HAPA tulikwama kidogo kwa muda...

Vyombo vya ujenzi wa barabara (magreda na makatapila) ndivyo vilivyokuwa vikitupa msaada wa kutukwamua......

 

 

Pamoja na yote hayo, lakini bado ni maeneo ya kuvutia kwa misitu ya mikorosho na nyumba za asili...

Ndio maana tunakuwa wakali kwa ajili ya gesi! Wewe mwenyewe si unaiona hii nyumba yetu, halafu ndio mnataka kutuacha vipi sasa!

 



Mji wa Somanga kwenye gesi. Tayari wamekwishaanza kuonja matunda ya gesi. Si unaziona hizo nyaya za umeme wa Gesi.

 


Kituo cha kulipatia chochote kitu tumbo katikati ya safari....

Hapa tumeshuka kwenye basi na kuanza kutawanyika huku na kule; wengine vyooni...wengine kwenye chai na wengine kwenye msosi... Lakini na wengine tulishuka ili tuzungukezunguke tu hapa na pale; mfukoni hakuna kitu!


Pembeni ya sehemu ya kujipatia msosi, pia wapo wakina mama wanaouza samaki wa kukaanga. Sikuwa na pesa ya kutosha mfukoni, huenda ningekununulia hata wawili watatu tu hivi ili nikutumie...ila wanauzwa bei ghali hao! Ha! Zaidi ya bei ya jogoo mkubwa! 

 

No comments: