TUENDELEE KUZURURA NDANI YA JIJI-DAR.
Hapa ni maeneo ya Kivukoni (Ferry). Mpini wa Shoka ulikuwa unakwenda kupanda kivuko (Ferry) kuelekea Kigambonino (Kigamboni). Mnara unaouona mbele yako ni rada ya kuongozea usalama wa vyombo vinavyopita baharini (ndani ya maji), na hasa meli. Sasa sielewi kama mitumbwi na ngalawa navyo pia vina mawasiliano yoyote na rada hii!
Hapa ndipo pa kupandia Kivuko (ferry)....Tsh 200/- tu kwa mtu mmoja.
Mpini Wa Shoka ndani ya MV MAGOGONI...
Tumejazana kibao! Uzuri wa kivuko (ferry) hiki cha Mv Magogoni ni kikubwa mno zaidi ya kile cha Mv Kigamboni. Kwa hivyo, kinasomba watu wa kutosha juu na chini; na vyombo vya usafiri humohumo. Ila wakati wa kupanda, wakwetu ni vema ukachunga mifuko yako; hapa wajanja (wazee wa ndole a.k.a fingermaster wako wa kutosha na wengine wamenyuka suti za maana na tai shingoni ili usiwashitukie!). Miye nilikaa juu kabisa na Bwana mdogo wangu, Khamis Idd, ili niweze kukunasia vizuri mbili tatu. Juu kabisa ya maandishi MV MGOGONI, ndipo alipo nahodha (dereva) wa kivuko.
HII ni MV KIGAMBONI...
Wakati sisi tukianza kuondoka na Mv Magogoni, Mv Kigamboni nayo ilikuwa inapakiza ili itufuate. Japo Mv Kigamboni ni ndogo, lakini inakwenda kwa kasi zaidi ya ile ya Mv Magogoni. Wakwetu, watu hawaogopi! Hivi huo mlango waliosimama juu yake kwa kujiamini, je minyororo iliyoushika ikifunguka ghafla ndiyo inakuwa ni nini! Kilio cha samaki, kesi kwa serikali...!
Ndani ya Mv Magogoni, Mpini Wa Shoka ukayanasa vizuri majengo pacha ya Benki Kuu ya Tanzania (B.O.T). Kushoto mwake, inaonekana hoteli ya Kilimanjaro. Raha!
Japokuwa jua lilikuwa ni kali kutokea upande huu, lakini Mpini Wa Shoka uliinasa hivyohivyo Bandari kuu ya Dar es salaam na miji-meli yake ya kila aina.
Hapa ni soko la Samaki-ferry. Mpini Wa Shoka ulilinasa kwa upande wa nyuma (upande wa baharini) wakati nikichanja mbuga kuelekea Kigamboni.
KIGAMBONI....
Ndiyo tunaanza kuisogelea taratiiiiiiiibu. Si unapaona mwenyewe kwa mbali. Kigambonino!
Hapa ndiyo tunateremka. Abiria chunga mfuko wako! Karibu Kigamboni. Usihofu; endelea tu kukodoa jicho, nitajitahidi tuzurure sote hapa na pale japo hata kidogo tu. Huu upara wa huyu jamaa hapa jirani kabisa, ni wa asili au ni wa kunyoa! Aisee, unawaka vilivyo.
No comments:
Post a Comment