Wakati mwingine unapokutana na tukio kama hili, unaweza ukajikuta ukicheka ghafla tu, bila ya kutarajia baada ya kugundua ni kitu gani hasa kinachoendelea! Kwa harakaharaka picha hizi utakazoziona hapa chini unaweza ukafikiri ni kama vile ni tukio la vibaka (wezi) fulani hivi wanaojaribu kuiba, lakini hapana. Hapa hakuna mwizi hata mmoja. Mpini wa Shoka ulishuhudia live. Hapa ni eneo la Nobo Haus (Noble House) mjini Arusha; ingawa wananchi wengi wamepazoea zaidi kwa jina la Jogoo Haus (Jogoo House). Ni jirani kabisa na Stendi Kuu ya Mabasi; na pia ni jirani sana na Soko Kuu. Zamani kidogo palikuwa ni maegesho ya mabasi ya Scandnavia (kwa sasa hayapo tena). Ni eneo lisiloruhusiwa kwa biashara yoyote ile ndogondogo (umachinga). Sasa kwa sababu ni eneo lenye wingi wa watu kutoka Stendi na Soko Kuu, wafanyabiashara ndogondogo wamekuwa wakitega bidhaa zao ili kuwanasa wateja kwa urahisi. Lakini panapotokea taarifa kwamba askari wa halmashauri ya jiji wameonekana mahali fulani na wanaelekea katika eneo hili, basi ndipo bidhaa huanza kuondolewa haraka haraka ili zisikamatwe. Na mojawapo ya mbinu inayotumika kuzihamisha bidhaa hizo ni kama hivi unavyoona hapa chini.....
Pochi na mabegi vinachomolewa harakaharaka kutoka kwenye uzio wa bati....
Kisha....
Yanarushwa kwa kasi upande wa pili wa uzio (ndani ya maegesho ya zamani ya mabasi ya Scandnavia). Unaweza ukafikiri hayo mabegi yaliyoko juu yamenasa tu kwenye nyaya za umeme! La hasha! Hayo yapo angani baada ya kurushwa, yakielekea kutua upande wa pili! Biashara Mjini; akili na mbinu ni kichwani mwako.
No comments:
Post a Comment