JE, WEWE UNAPENDA KUJISOMEA VITABU?

Kama kuna jambo linaloleta changamoto, ufumbuzi, mbinu, harakati na ujuzi mwingi na wa aina yake, basi ni sanaa ya usomaji wa vitabu. Usomaji wa vitabu ni chemchemi ya kujua na kujifunza mambo na masuala mengi mno. Kiwe ni kitabu cha Hadithi, Riwaya au ni cha taaluma (elimu) fulani hivi, basi ni lazima tu kwa msomaji atapata kitu fulani kipya na cha muhimu sana ndani ubongo wake.

 

Mpini Wa Shoka ulimnasa kijana huyu, Fredy Gredson (Ras) wa Kata ya Daraja Mbili Jijini Arusha akiwa ametulia tuli ndani ya utulivu wa kutosha akisoma mojawapo ya vitabu vya Riwaya ya Kiswahili mbele ya ofisi yake anayoisimamia, ya ukusanyaji na uuzaji wa chuma chakavu (scraper). Je, na wewe  unaonaje kama utaanza kujijengea kaji-utaratibu ka-kuanza kujisomea kitabu angalau kimoja tu hadi ukimalize kabisa, ili upate maarifa, ujuzi na burudani ya kutosha kama alivyo kijana huyu?




Hapa kijana Fredy Gredson (Ras) akiendelea kukisoma kitabu chake huku pembeni yake akiwa amekaa mmoja wa marafiki zake wa kikazi, Saidi Khalifa (Saidoo). Sasa sielewi hapa Fredy alikuwa akisoma kwa sauti ya juu na Saidi akimsikiliza kwa makini, ama vipi! Mimi sijui! Utamu wa kitabu, ni ukisome ama usimuliwe kwa ufasaha na kwa utulivu wa kutosha, ndipo utapouhisi uhondo wake.




Hizi ni baadhi ya bidhaa (vyuma chakavu) pamoja na mzani wa kupimia kwenye ofisi anayoisimamia kijana Fredy Gredson (Ras). Ni ofisi ambayo imelikusanya kwa pamoja kundi kubwa la vijana mchanganyiko katika Kata hii ya Daraja Mbili, Jijini Arusha chini ya usimamizi wa bosi wao, Bwana Ferii…

No comments: