KAMA WEWE NI MMOJA WA WALE AMBAO WAMEKWISHA KUBAHATIKA KUHUDHURIA TUKIO KAMA HILI MAHALI POPOTE PALE UNAPOPAJUA, NA MOYO WAKO HADI LEO HAUJAWEZA KUPATA FUNZO LOLOTE LILE JUU YA MAISHA NA UHAI WAKO HAPA DUNIANI, BASI WEWE KWA HAKIKA YAWEZEKANA HAPATOKUWA NA JAMBO JINGINE LOLOTE LILE ZITO CHINI YA JUA LITAKALOUPA FUNZO MOYO WAKO! LABDA NI HADI PALE KIFO 'kitakapokuvamia' GHAFLA TU!
Hii ni mojawapo ya 'nyumba za milele' za miezi ya hivi karibuni tu kwenye makaburi ya Ngaramtoni ya Chini, jijini Arusha. Ndani ya tuta hili la kaburi lililomwagiwa maji kwa juu, amelazwa rafiki yangu mkubwa, mjomba wa mke wangu, 'Anko Abdillahi', ambaye kabla ya kifo chake, naye alikuwa na mipango na mikakati yake chungu nzima ya kimaendeleo na ya kifamilia kama ilivyo kwa mimi na wewe. Lakini, masikini malengo na mikakati yake yote ilikatishwa ghafla na kifo! Je wewe na mimi ni kipi kinachozidanganya nafsi zetu kwamba, sisi kwa upande wetu haipo kamwe sekunde tusiyoijua ambapo kifo 'kitatuzimisha' ghafla tu na kutufanya tulazwe ndani ya 'nyumba ya milele' kama hii alimolazwa Anko Abdillahi wa Ngaramtoni ya Chini! Au kama 'alivyozimika' ghafla tu hivi karibuni mwanamuziki maarufu wa Tanzania, Albert Mangweha 'Mang Air', aliyefia nchini Afrika Kusini! Na hebu watazame watu katika picha hii. Je, unamwona hata mmoja anayebaki tena ili aishi na marehemu hapa! Hakuna. Kila mmoja anaelekea kwenye pilikapilika zake za kidunia. Na baada ya siku chache, hata kama wewe ni maarufu kwa kiwango gani, wataanza kukusahau polepole... na mwishowe, watakusahau kabisa! Ni heri kujinyenyekeza na kumsujudia Bwana Mungu wako wakati ungali hai hapa duniani kama alivyosema Yesu wa Nazareti; maana hata Mpini Wa Shoka haujui kamwe kama ndani ya kaburi ipo tena nafasi kama hiyo! Ni vema kutoyajadili na kuyazungumza sana ya marehemu hapa duniani, bali ni vizuri kuijadili na kuitazama nafsi yako wewe binafsi kama ina nafasi au lolote lile la maana ililolitanguliza mbele za Mungu endapo kifo 'kitakusomba' ghafla tu hata dakika hii!
No comments:
Post a Comment